KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amesema ili timu iweze kutwaa ubingwa wa msimu huu inatakiwa isipoteze "hesabu" zake kwa kutoruhusu kupoteza pointi katika kila mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inatarajiwa kuendelea tena Novemba 18, mwaka huu.
Akizungumza na gazeti la Nipashe, Omog, alisema mbali na timu kushinda, vile vile unatakiwa kuwaombea dua mbaya ya kupata matokeo mabaya wapinzani wako katika mechi zao wanazocheza kwenye ligi hiyo ya juu nchini.
Kocha huyo wa Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, alisema endapo hilo likatokea, litasaidia kupunguza hofu na presha katika kila mechi kwa sababu tofauti ya pointi itakuwa kubwa ukilinganisha na ilivyo sasa kwenye msimamo wa ligi.
"Ligi ni ngumu na inaimarika kila raundi, hakuna kulala na ili utimize malengo ni lazima usipoteze hesabu, hii ninamaanisha usikubali kupoteza pointi, lakini pia ukiomba wapinzani wako wapate matokeo mabaya, kwa msimu huu, timu shindani ziko tano, hali ni ngumu na imeongeza changamoto," alisema Omog.
Kuhusu kucheza mechi za kirafiki mfululizo, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Masoud Djuma, alisema kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa sababu ya kuwapa nafasi wachezaji wasiocheza kujiimarisha na kuwa tayari kupambana kwenye ligi.
"Hatutapumzika, tumekubali kucheza mechi za kirafiki ili kuwanyanyua wachezaji ambao bado wako chini, hii inatusaidia kiufundi, tunataka kuona kila mmoja anapata nafasi ya kucheza, wanazunguka, tunaamini uamuzi huu utatusaidia huko mbele tunakoelekea," alisema Djuma.
Kocha huyo aliongeza kuwa tangu ajiunge na Simba kuna idara ambazo alizikuta dhaifu na sasa zimeanza kuimarika huku pia akisema wameshaanza kujadiliana kuhusu kuimarisha kikosi hicho wakati wa dirisha dogo la usajili.
Baada ya juzi kutoka sare ya bila kufungana katika mechi ya kirafiki na timu ya Nyundo FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili mkoa wa Katavi, kikosi cha Simba jana mchana kilitua Sumbawanga Mjini kuweka kambi ya muda na Jumamosi kitacheza mchezo mwingine wa kirafiki ulioandaliwa na wenyeji wao.



Post A Comment: