Mshambuliaji Saimon Msuva alifunga bao la ufundi mkubwa wakati timu yake Difaa El Jadida ikikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Wydad Casablanca ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’.
Msuva alifunga bao lake akiunganisha kwa shuti la moja kwa moja mpira kichwa uliopigwa na beki wa Wydad aliyejaribu kuokoa mpira huo.
Mshambuliaji huyo amekuwa na mafanikio makubwa tangu alipotua El Jadida akitokea Yanga mwisho wa msimu uliopita.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha mkuu wa Difaa, Abderrahim Talib baada ya kuongozwa kwa mabao 2-0 kwa kuwatoa Mario Mandrault, Bilal El Magri na nafasi zao kuchukuliwa na Tarik Astati, Hamid Ahadad yalionekana kuwa na tija kwa Msuva kufunga bao la kufutia machozi.
Hicho ni kipigo cha pili kwa Msuva kukipata ndani ya siku tano baada ya kufungwa kwa penalty 3-1 mwishoni mwa wiki katika Kombe la Mfalme dhidi ya Raja Casablanca.
Difaa itacheza tena ugenini, Novemba 26 kwenye uwanja wa Stade Père-Jégo (Casablanca) na wenyeji wao, Racing de Casablanca, majira ya saa 12;00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.



Post A Comment: