ads

MSHAMBULIAJI wa Simba, Laudit Mavugo, amemwaga siri za ndani ya kikosi chao akisema kuwa pamoja na presha ya mashabiki wao wanaoonekana kuwa na usongo wa ubingwa, wao kama wachezaji hawana mchecheto ng’o wakifahamu iwe isiwe, lazima taji la Ligi Kuu Tanzania Bara litue Msimbazi msimu huu.


Kutokana na hilo, amewatuliza mashabiki wao kwa kuwataka kuondoa hofu kwani wao kama wachezaji, wanajua nini wanachokifanya ndio maana haikuwa shida kwao juzi kuwachapa Stand United mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga.

Katika mchezo huo, mabao ya Simba yaliwekwa nyavuni na Shiza Kichuya dakika ya 17 na Laudit Mavugo dakika ya 47, huku bao pekee la Stand United likifungwa na Muhajhe Mtasa, dakika ya 51.

Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 11, sawa na Mtibwa Sugar na Azam, lakini Wekundu wa Msimbazi hao wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi kutokana na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Wakati Simba wakiwa na mabao ya kufunga 14 na kufungwa matatu, Mtibwa wamecheka na nyavu mara tano na kupigwa mawili, huku Azam ikiwa imejikusanyia mabao manne na nyavu zao kutikiswa mara moja.

Akizungumza na gazeti la  BINGWA jana, Mavugo alisema: “Mashabiki wasiwe na wasiwasi, unajua mpira una matokeo matatu; kufungwa, kushinda au kutoka sare, hilo lazima wajue… wasiwe wepesi kutupa lawama pale tunapofanya vibaya, waendelee kutupa moyo, hatuwezi kuwaangusha.”

Alisema tatizo la umaliziaji wa mabao ambalo limekuwa likiisumbua timu hiyo wameanza kulifanyia kazi kwani katika michezo miwili waliyocheza dhidi ya Mbao FC na Stand United, wamefunga mabao kuanzia mawili.

“Nikifunga mimi au akifunga Okwi na mwingine yeyote sawa tu, sisi ni timu moja na uzuri ni kwamba tumeanza kuelewana katika kutumia mifumo mbalimbali, nina uhakika kuna mambo mazuri yanakuja huko mbeleni zaidi ya haya,” alisisitiza Mavugo.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: