Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam, wamewahoji kwa zaidi ya saa sita, madiwani waliojiuzulu Chadema wanaotuhumiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari kuwa walipewa rushwa.


Waliofika Takukuru ni Catherine Mtui, aliyekuwa diwani wa viti maalumu, Japhet Jackson (aliyekuwa diwani wa Ambuleni) na Bryson Isangya (aliyekuwa diwani wa Maroroni). Baada ya kuhojiwa hawakutaka kuzungumza chochote wakisema wanaacha uchunguzi uendelee.

Pamoja nao, diwani wa Mbuguni, Ahimidiwe Rico anayedaiwa kuwa ndiye alirekodi sauti na picha wakati akishawishiwa na viongozi wa Serikali na wa Halmashauri ya Meru amehojiwa kwa zaidi ya saa tatu jana Jumanne Oktoba 17, 2017.

Rico amesema amewaeleza Takukuru kila kitu ambacho anakifahamu katika sakata hilo, ikiwemo kuwarekodi viongozi ambao walimshawishi kujiuzuru udiwani.

"Msimamo wangu ni kwamba, nachukia rushwa. Nimewaeleza kila kitu na wao waliniuliza kuhusu vifaa nilivyotumia kuwarekodi nikawaambia ni mali ya mbunge, alivitoa nchini Uingereza," amesema.

Rico aliyesindikizwa na diwani wa  Nkwanankore, Wilson Nanyaro amesema  ana imani na Takukuru kwamba watafanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua.


"Nimewaeleza wazi kuwa hata shauri hili likienda mahakamani nipo tayari kwenda kutoa ushahidi na kuthibitisha sauti za watu ambao niliwarekodi," amesema.

Amesema baada ya mahojiano yaliyoanza saa tatu hadi saa sita mchana, maofisa wa Takukuru wamemwambia aondoke na watamuita watakapomuhitaji.

Hakuna ofisa wa Takukuru aliyekuwa tayari kuzungumzia mahojiano hao wakisema wasemaji ni makao makuu ya ofisi hiyo Dar yaliyoko jijini Dar es Salaam.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: