KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni kutofurahishwa na tabia ya baadhi ya watu wanaotumia vibaya mitandao wakitumia jina lake, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amefunguka na kutaka watu hao wapuuzwe.
Hivi karibuni, baadhi ya watu wamekuwa wakifungua akaunti bandia wanazozitambulisha kwa majina yanayoshabihiana na rais huyo mstaafu na kisha kutoa maoni kuhusiana na masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.
Alipokuwa akimwapisha Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma, Rais Magufuli aliwapongeza majaji wakuu wastaafu kwa uadilifu wao unaowafanya wasizungumze chochote huku akiwaelezea wastaafu wasiochoka kusema kuwa ni wenye ‘kuwashwawashwa’.
Licha ya Rais kueleza hayo, baadhi ya watu waliendelea kutumia akaunti bandia zenye majina ya Kikwete kutoa maoni mbalimbali yakiwamo yanayoonekana kuipinga serikali.
Katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais huyo mstaafu jana, Kikwete aliwataka Watanzania wapuuze watu hao kwa kuwa maneno wanayoandika hajawahi kuyatamka.
“Watu hao wamekuwa wakimlisha maneno ambayo hajayasema. Rais mstaafu amesikitishwa sana na uvumi huo juu yake, hivyo wadau na wananchi wengine wanapaswa kupuuza maneno hayo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo, ikimnukuu Kikwete.
Katika taarifa hiyo, wananchi wameombwa kupuuza uzushi wa taarifa mbalimbali zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia maneno ambayo hajawahi kuyatoa.
Baadhi ya nukuu ‘feki’ ambazo zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kuhusisha akaunti bandia zenye jina lake ni pamoja na zile zinazogusa masuala ya kisiasa na ya kiusalama.
Mojawapo ya maoni hayo yaliyosambazwa kupitia akaunti bandia zenye jina la Kikwete, na ambayo ofisi ya Kikwete imeitaja kuwa mfano, ni ile iliyoandika:
“Pale unapomuona mtu anajaribu kumlazimisha mbwa asibweke wakati ni sehemu ya maisha yake kubweka, lazima utajiuliza huyu mtu hutumia nini wakati wa kufikiri.
Lakini naomba mtambue kuwa unapokuwa kiongozi usipokuwa na busara na kuheshimu maoni ya watu wa pembeni yako utahishia kuwamaliza viongozi wenzako ukihisi ni maadui.”
Taarifa hiyo ilifafanua zaidi kuwa maneno hayo hayajasemwa na Rais mstaafu (Kikwete) na kwamba, Kikwete amesikitishwa na uzushi huo.
“Wananchi na wadau wengine mnataarifiwa kupuuza maneno hayo,” ilieleza taarifa hiyo.



Post A Comment: