ads

IMEELEZWA kuwa moyo wa huruma ni moja ya sababu nne zinazofanya idadi ya wanawake waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa waliopo katika magereza nchini kuwa ndogo kuliko wanaume.


Kati ya wafungwa 465 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa hadi miaka miwili iliyopita, ni 20 tu ambao ni wanawake kwa mujibu wa takwimu zilizopo.

Idadi ya wafungwa wanaosubiri kunyongwa hadi kufa inatarajiwa kuongezeka tangu hapo baada ya Rais John Magufuli kumuomba Jaji Mkuu, Prof Ibrahim Juma kutopemlekea orodha ya watu wanaopaswa kunyongwa, katika utawala wake, alipomuapisha Ikulu wiki mbili zilizopita.

Rais Magufuli alisema hayupo tayari kutia sahihi utekelezaji wa hukumu ya kifo dhidi yao, kitendo ambacho hakijafanyika kwa awamu mbili zilizopita za serikali pia.

Alisema anatambua ugumu wa kutekeleza adhabu hiyo, hivyo akaitaka mahakama kutompelekea orodha ya waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa.

"Kazi ya ujaji mkuu ni kazi ngumu, mojawapo ni kuhukumu kunyonga, kama ambavyo mmekuwa mkifanya. Mnapoleta kwetu kwa wanasiasa tunaogopa kuidhinisha kunyonga," alisema na kueleza zaidi:

"Na ninaambiwa wapo wengi tu walioidhinishwa kunyongwa, lakini naomba hiyo orodha wala msiniletee kwa sababu ninajua ugumu wake ulivyo."

Ripoti ya Tume za Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyotolewa Mei 2015, ilibainishwa kuwa kuna Watanzania 465 wanaosubiri kunyongwa katika magereza mbalimbali nchini.

Pia Ripoti ya Mpango wa Kujitathmini kuhusu Haki na Utekelezaji wa Haki za Binadamu (UPR), unaotekelezwa kwa mara ya pili nchini, inaonyesha kuwa kuna wafungwa 465 wanaosubiri adhabu ya kifo, kati ya hao wanaume ni 445 na wanawake ni 20.

Mwanasaikolojia Dk. Peter Mitimingi alisema zipo sababu kubwa nne ambazo zinasababisha wanaume kuchukua maamuzi magumu kuliko wanawake, na hivyo idadi ya watu walio katika orodha ya kunyongwa hadi kufa kuonyesha wanawake wachache.

Alisema sababu hizo ni huruma, mfumo wa mapokeo ndani ya jamii, msongo wa mawazo na ujasiri.

Alisema ndani ya jamii inaaminika kuwa mwanaume anatakiwa kuwa jasiri, sugu tangu akiwa mdogo na kwamba kiasili mwanamke ana uwezo wa kutoa 'kitu' kilicho moyoni mwake kuliko mwanaume.

"Pia ujio wa utandawazi umezidisha haya matukio, kuangalia picha za ukatili, mauaji inajenga dhana mbaya," alisema Dk. Mitimingi.

"Mwanaume anapokuwa na msongo (wa mawazo), hamwambii mtu mengine, anameza na kuishia kujeruhi moyo na kusababisha kuwa na hasira, hisia kali na kufanya maamuzi mabaya."

Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sura ya 6 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, inatoa adhabu ya kifo kwa makosa ya uhaini, ugaidi na kuua kwa kukusudia.

Lakini pamoja na kuwapo kwa kifungu hicho, adhabu hiyo haijatekelezwa kwa wafungwa waliohukumiwa tangu mwaka 1994.

Rais wa tatu, Benjamin Mkapa na mrithi wake, Jakaya Kikwete hawakutia sahihi hati za kunyonga mpaka kufa na sasa Rais wa tano ameendeleza hali hiyo.

Credit - Nipashe.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: