WATU wanne wamefikishwa mahakamani nchini Afrika Kusini wakikabiliwa na mashtaka ya kula nyama za watu baada ya mtu mmoja yao kwenda katika kituo kimoja cha polisi na kusema kuwa amechoka kula nyama za watu.
Alipohojiwa zaidi, mtu huyo alitoa sehemu ya mguu wa binadamu pamoja na mkono.
Polisi waliamua kumsindikiza mwanaume huyo kwenda katika nyumba moja huko KwaZulu-Natal ambapo sehemu zaidi za miili ya binadamu ilipatikana.
Watu wanne, wawili kati yao wakiwa ni waganga wa kienyeji, awalikamatwa na kushtakiwa kwa mauaji na kula njama za kuua.
Walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi ya Estcourt, kilomita 175 kaskazini mashariki mwa jiji la Durban Jumatatu 21/08/2017.
Msemaji wa polisi aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC kwamba inawezekana kwamba vijana hao wanne, wenye umri kati ya miaka 22 na 32, ni sehemu ya mtandao mkubwa wa watu wanaojihusisha na suala hilo.
Uchunguzi bado unaendelea, huku polisi wakiwataka watu ambao ndugu zao wamepotea katika maeneo ya Estcourt kujitokeza.
Wataalamu wa polisi wameitwa ili kujaribu kutambua masalia ya watu, kwa kuwa haijulikani kama sehemu hizo za mwili ni za mtu mmoja au watu kadhaa.
Mwezi mmoja uliopita, katika jiji la Durban, mtu mmoja alikamatwa akiwa na kichwa cha mtu, akiwa amekiweka katika begi la mgongoni. Inaaminika kwamba alikuwa anajaribu kuuza kichwa hicho kwa mganga wa kienyeji.



Post A Comment: