Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amekataa kubadilishiwa msaidizi wake na badala yake kulazimisha Mganda Jackson Mayanja, aendelee kubaki katika nafasi yake ile ile, imebainika.
Kutokana na uamuzi huo, Omog pamoja na Mayanja jana asubuhi walisimamia mazoezi ya timu hiyo ambayo yalifanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi kilichoko barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Taarifa kutoka ndani ya klabu ya Simba zilieleza kuwa Omog hakuwa tayari kuona Mayanja anaondolewa na kumtaka Mganda huyo kufika mazoezini jana kama kawaida kwa ajili ya kuanza programu yao waliyoiandaa kuelekea msimu mpya wa 2017/18.
Kocha ambaye anatajwa kushika nafasi ya Mayanja ni Mrundi Etienne Nyayiragije, ambaye msimu uliopita aliiongoza Mbao FC ya Mwanza.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mayanja, alisema hajafahamu hatima ya ajira yake kwa sababu bado anaendelea na mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo ambayo mwakani itashiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.
"Ni kweli leo (jana) nilikuwa mazoezini, lakini bado niko katika mazungumzo na viongozi, sijajua wataamua nini, ila nimewaambia kila kitu ninachokihitaji kwa upande wangu," Mayanja alisema kwa kifupi.
Wakati huo huo kiungo wa kimataifa wa Simba kutoka Ghana, James Kotei, alitarajiwa kurejea nchini jana usiku kwa ajili ya kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Pia taarifa kutoka Simba zinaeleza kuwa mshambuliaji wake kutoka Burundi, Laudit Mavugo, anatarajiwa kurejea nchini leo na wote wataungana na wenzao katika maandalizi ya msimu mpya kuanzia kesho.
Kikosi cha Simba kinatarajia kwenda Afrika Kusini kuweka kambi kujiandaa na msimu mpya na kitarejea nchini siku chache kabla ya Tamasha la Simba Day ambalo litafanyika Agosti 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.



Post A Comment: