ads

JESHI la Wananchi (JWTZ) limekabidhi majengo yaliyokarabatiwa kufuatia tetemeko la ardhi la Septemba 10, mwaka jana katika wilaya za Missenyi, Bukoba Mjini na Bukoba, ikiwa ni jitihada za serikali za kurudisha miundombinu iliyoharibiwa.


Akizungumza katika makabidhiano hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenister Mhagama alisema kurejea kwa huduma za zahanati kutaleta maendeleo katika kijiji cha Kabyaile na kusifu uzalendo ulioonyeshwa na JWTZ   na vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). 

“Vijana mtakuwa mmepata fundisho na elimu kupitia hawa vijana wenzenu wa JKT walivyojitoa kizalendo kuwajengea zahanati,” alisema Mhagama akiwaambia wakazi wa kijiji hicho.

Jeshi hilo lilikabidhi majengo 11 ya zahanati juzi ambayo yametumia Sh. bilioni 1.7 na ujenzi wake umechukua miezi nane hadi kukamilika.

Waziri huyo alisema ujenzi huo ni agizo la Rais John Magufuli baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi.

Naye Mwakilishi wa JWTZ kutoka makao makuu, Sylvester Ghuriku, alisema majengo hayo yatumike vizuri ili watu wote wanufaike na huduma zitakazotolewa. 

“Niombe tu majengo haya yatumike vizuri pamoja na kutunzwa ili vizazi vijavyo viweze kutumia huduma zake,” alisema Ghuriku. 

Aliongeza kuwa Jeshi hilo litaendelea kushiriki shughuli za kuwasaidia wananchi wakati wa matatizo.

Mkuu wa kikosi kilichokuwa kikijenga majengo hayo, Meja Buchard Kakula, alisema majengo hayo yatatumika kutolea huduma ya kwanza, sehemu ya kuchomea sindano, sehemu ya kulazia wagonjwa, chumba cha mochwari na nyumba moja ya wauguzi.

Kakula alisema licha ya kukamilika kwa majengo hayo sehemu za ndani, bado mazingira ya nje hayajakamilika kwa kuweka uzio, mifereji ya maji yanayotiririshwa na mvua na njia za kupitia.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: