Rais John Magufuli ameshtukia ubadhirifu wa Sh42 bilioni kwenye fedha za pembejeo za kilimo baada ya kuelezwa kwamba Serikali inadaiwa Sh50 bilioni, lakini baada ya uhakiki kwenye mikoa 11 ilibainika madai halali ni Sh8 bilioni.
Alisema Serikali itafanya uhakiki nchi nzima kwenye fedha za ruzuku na pembejeo za kilimo, baada ya kugundua njama za kuongeza majina ya watu wasiostahiki kupata fedha hizo wakiwamo marehemu.
Rais Magufuli alisema hayo juzi wilayani Chato mkoani Geita kwenye hafla ya kukabidhi nyumba 50 kati ya 450, zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa.
Nyumba zilizokabidhiwa, 20 ziko Geita, 10 ziko Kagera na 20 ziko Simiyu.
Alisisitiza kwamba tatizo la ubadhirifu wa fedha za umma limeenea kwenye halmashauri zote nchini.
Rais Magufuli alizitaka halmashauri hizo kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za Watanzania kwa kuhakikisha zinafanya kazi katika maeneo yaliyokusudiwa.
Mkuu huyo wa nchi aliwataka viongozi wa Serikali kufanya kazi kwa uzalendo na kusimamia vizuri fedha.
Alisema mgogoro mkubwa upo kwenye fedha za ruzuku ya pembejeo za kilimo na watu waliokufa nao wameorodheshwa kuzipata.
“Na wanaohusika wengine ni viongozi, viongozi wa ndani ya Serikali na viongozi ndani ya halmashauri. Hata hapa Chato, sitaki nizungumzie sana, sifahamu kama kesi imekwisha, fedha za pembejeo zililiwa Sh1.5 bilioni,” alisema Rais Magufuli.
Alisema siku moja alimuuliza mama yake “mama mbona nawe uko kwenye orodha, ulichukua vocha?” yeye akafikiri vocha ni ile ambayo wanamnunulia wajukuu zake kuweka kwenye simu. Alisisitiza kwamba mchezo huo uko karibu kila mahali.
“Tunafanya auditing ya Tanzania nzima, nayo tutayasema hadharani. Pamekuwa na hewa nyingi, mara uhangaike na hewa ya wafanyakazi, hewa ya watu wa elimu feki, hewa ya Tasaf lakini niwaombe viongozi wote Tanzania, tushirikiane,” alisema Rais Magufuli.
Aliwataka viongozi kuiga mfano wa Taasisi ya Mkapa katika kutekeleza miradi kwenye halmashauri zao. Aliwapongeza wakandarasi kwa kutekeleza ujenzi wa nyumba hizo ndani ya wakati na kwa ubora.
Rais Magufuli alisisitiza kwamba ataendelea kuwa upande wa Watanzania hasa wale maskini, ndiyo maana Serikali imepunguza bei ya dawa na ushuru wa mazao kwa wakulima.
“Mwaka huu kwa mfano, kupitia Bunge, tumetoa na kufuta tozo zaidi ya 80 kwenye kilimo, tozo zaidi ya saba kwenye mifugo na tozo zaidi ya tano kwenye uvuvi. Kwenye kilimo ilikuwa ukitoka na gunia moja lazima ulipe ushuru lakini sasa ukitoka na tani moja kutoka wilaya moja kwenda nyingine utapita bure,” alisema Rais Magufuli.



Post A Comment: