Chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta kimeeleza wasiwasi wake dhidi ya muungano wa upinzani wa Nasa kuweka kituo cha kujulisha kura nchini Tanzania.
Hata hivyo, Serikali nchini ilishakanusha kuhusu kuwapo mpango huo na kwamba, haitaruhusu hilo kufanyika.
Vyombo vya habari vya Kenya juzi na jana vimeripoti kuhusu kuwapo kituo hicho cha Nasa nchini.
Baadhi ya wabunge wa Jubilee wakiwa katika kampeni juzi wametoa shutuma hizo wakizielekeza kwa Rais John Magufuli kwamba, kituo hicho kitawekwa nchini kutokana na ukaribu wake na mgombea wa Nasa, Raila Odinga.
Wiki iliyopita, mgombea urais wa muungano wa Thirdway Alliance, Dk Ekuru Aukot naye ameeleza wasiwasi huo.
Ujumbe wa Jubilee ukiongozwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho, David Muthare ambaye ni rafiki wa karibu wa Rais Kenyatta pia amezungumzia taarifa za uwepo wa kituo hicho.
Tuhuma hizo zinatolewa zikihusishwa na tukio lililotokea nchini Gambia mapema mwaka huu, ambako aliyekuwa mgombea urais, Adama Barrrow alitangazwa mshindi katika nchi jirani ya Senegal baada ya mpinzani wake aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Yahya Jameh kupinga matokeo.
Rais Magufuli kabla ya kushika wadhifa huo, amehudhuria kongamano la ODM katika uwanja wa Kasarani lililomwidhinisha Raila Odinga kuwa mgombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2013.
Magufuli pia amehudhuria maziko ya mtoto wa kwanza wa Raila, Fidel Odinga yaliyofanyika eneo la Bondo miaka miwili iliyopita.
Baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka 2015, Raila amekuwa kiongozi wa kwanza wa kimataifa kumtembelea Rais Magufuli nyumbani kwake wilayani Chato.
Licha ya Serikali nchini kukanusha kuwapo kwa kituo hicho, wiki iliyopita kiongozi mwenza wa Nasa na seneta wa Bungoma, Moses Wetang’ula amesema madai ya kuwekwa kituo Tanzania ni dalili ya kuweweseka kwa Serikali kwa sababu inajua upinzani watashinda uchaguzi utakaofanyika Agosti 8.
Post A Comment: