Ilikuwa ni zaidi ya harusi wakati mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule aliposherehekea harusi yake na mchumba wake wa siku nyingi, Grace Mgonjo kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, nyota wa muziki Tanzania, Diamond Platnumz, malkia wa R&B, Lady Jay Dee, wanasiasa na watu wengine maarufu ni miongoni mwa waalikwa walioifanya sherehe hiyo kuwa ya aina yake.
Pia alikuwapo James Mbatia, ambaye ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na mbunge wa Vunjo na wabunge wengine, Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini, Chadema), Godbless Lema (Arusha Mjini, Chadema) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini, Chadema).
Tofauti za kisiasa ziliwekwa kando katika harusi hiyo wakati mbunge wa Kondoa Mjini (CCM), Edwin Sanga na mkewe pamoja na Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini, CCM) walipoungana na wageni wengine kusherehekea harusi hiyo, iliyofanikishwa na kamati iliyoongozwa na Mapunda.
Pamoja na watu hao maarufu, hata burudani ilikuwa ya wasanii maarufu. Diamond, Lady Jay Dee, Mbilinyi, anayejulikana kisanii kwa jina la Mr ll au Sugu na Haule ambaye pia anajulikana kwa jina la Profesa Jay, waliamsha watu kudansi kwa nyakati tofauti.
Ndoa hiyo ilifungwa katika Kanisa la St Peter, Oysterbay Dar es Salaam kabla ya kuhamia Mlimani City. Mr 11, Msigwa na wenzake watatu waliingia ukumbini na wimbo wa Doro Bucci wa Don Jazz. Ukumbi ulizizima kwa shangwe baada ya Profesa Jay mwenyewe kuingia ukumbini akimuimbia mke wake, wimbo wa ‘Nipo kamili gado’. “This is love (huu ni upendo) kabisa mbele za Mungu,” alisema Haule alipozungumza na Mwananchi kuhusu harusi hiyo muda mfupi kabla ya kwenda fungate Hoteli ya Serena.
“Hii love sijawahi kuona. Ime cement (imeimarisha) maisha yangu mapya. Nimegundua hawa watu wananipenda, wananiamini.”
Haule, alisema pamoja na kuhudhuria harusi nyingi, hajawahi kuona hafla ambayo si ya kiserikali iliyohudhuriwa na wabunge wengi kama harusi yake.
Amesema harusi yake ilikuwa na mawaziri wakubwa, manaibu waziri, wabunge wa Chadema, CUF na wa CCM.
“ Sijapata support (sijasaidiwa) na wabunge wa upinzani tu. Wapo wengi sana wa CCM, ambao wamehudhuria na wamechanga. Kikubwa ni kwamba hakukuwa na tofauti za kiitikadi katika hili kwa sababu hata best man (msimamizi) wangu ni wa CCM, na mwenyekiti wa kamati yangu ya harusi ni Mapunda,” alisema Profesa Jay.
“Hiyo ni ishara kuwa tuna umoja, hakukuwa na itikadi, hicho ndicho kitu kikubwa. Kuna wakati watu wanatuangalia kama tuna ugomvi, lakini nashukuru wabunge wa vyama vyote wamejitokeza. Japo walitakiwa kwenda majimboni, walikuja kwenye harusi. Walikuwa na kazi zao, lakini wakasema wacha tum-support huyu jamaa.”
Kuhusu idadi ya wabunge waliohudhuria, Profesa Jay alisema kati ya wabunge 364 waliochanga, ni wabunge 50 tu ndio walioshindwa kuhudhuria sherehe ya harusi hiyo iliyokuwa na zaidi ya wageni 600.
Diamond, Mbowe, Lowassa, Jide
Harusi hiyo pia ilikuwa ya aina yake kutokana na ushiriki wa Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe waliokuwa kivutio.
Profesa Jay alisema Diamond hakuja peke yake, alikuwa na Kundi la Wasafi (WCB), akiwamo Harmonize, Rayvanny na wengine.
“Hebu fikiria, hawa watu wamechanga, wamehudhuria kisha wakafanya show bure (wakatumbuiza). Hicho kilikuwa kitu maalumu kwangu. Mtu kama Sugu au AY ku-perfom bure, si unajua mtu angeenda kwenye hiyo show ingekuwa shilingi ngapi?” Alihoji.



Post A Comment: