TANGAWIZI ina raha yake kwa wanandoa, hasa pale inapotumiwa kupitia kinywaji cha chai. Uchunguzi uliofanywa na gazeti la  Nipashe umebaini kuwa kiungo hicho, kwa sasa ni mojawapao ya habari kubwa mjini, hususan kwa wafuatiliaji wa masuala ya lishe.


Imebainika kupitia uchunguzi huo kwenye maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam kuwa kiungo hicho kimekuwa kikipata watumiaji wengi kila uchao kutokana na ukweli kuwa chenyewe, husaidia mno kuimarisha afya ya uzazi kwa kina baba.

“Watumiaji wa tangawizi wamekuwa wakiongezeka katika siku za hivi karibuni baada ya kubainika kuwa kinywaji chenye kiungo hicho husaidia kuongeza furaha ya ndoa…ni kwa sababu huwasaidia sana kina baba katika masuala hayo ya kuwaongezea ujabali katika mapenzi,” mmoja wa wauzaji maarufu wa tangawizi katika soko la Buguruni aliiambia Nipashe kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Aidha, imefahamika kuwa mbali na kusaidia masuala ya mapenzi kwa kina baba na hivyo kuwapa raha kwa kunogesha ndoa zao, kiungo cha tangawizi pia kimejaaliwa kuwa na viinilishe vyenye kuongeza kinga mwilini mwa watumiaji dhidi ya magonjwa mbalimbali.

UFAFANUZI WA KITAALAMU
Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki hii, mtaalamu wa Chakula na Lishe katika taasisi moja binafsi , Linus Gedi, alisema chai ya tangawizi imejaa utajiri wa virutubisho ambavyo ni kinga na tiba ya magonjwa mbalimbali ikiwamo ya kuimarisha ubora wa mbegu za kiume.

Alisema tangawizi imesheheni virutubisho kama madini ya potassium na manganese ambayo ni muhimu katika kuongeza mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Pia alisema tangawizi ina vitamin A, C, E, B-complex, chuma, magnesium, zinki, sodium, calcium, beta-corotene na phosphorus ambazo kwa pamoja, zote ni muhimu kwa afya ya mlaji.

Aidha, alisema unywaji wa chai ya tangawizi husaidia umeng’enyaji wa madini ya calcium na pia kinywaji hicho huwa na madini ya silicon ambayo kazi yake ni kuongeza afya ya nywele, ngozi, meno na kucha.

Gedi alisema kutokana na utajiri wa virutubisho mbalimbali ndani ya tangawizi, mtumiaji huuepusha mwili wake dhidi ya mashambulizi ya magonjwa.

“Endapo tangawizi itatumiwa mara kwa mara, itamsaidia (mlaji mwanaume) kuboresha mbegu za kiume na nguvu za uzazi kwa wanaume…hili husaidia kutibu upungufu wa nguvu za kiume,” alisema Gedi.

Alisema kwa wanawake wajawazito, chai ya tangawizi inapotumiwa huwasaidia kuwaondolea kichefuchefu kinachosababishwa, hasa asubuhi.

“Chai ya tangawizi inaweza kuzuia kutapika na kumaliza maumivu ya kichwa, pia inazuia kichefuchefu kinachotokana na mitingishiko ya safari za ndege, meli au gari… unaweza kunywa kikombe kimoja cha chai (ya tangawizi).

“Ndio maana tunashauri watu wajenge tabia ya kutumia kiungo hiki kwenye vyakula,” alisema Gedi.

Pia alisema chai ya tangawizi husaidia mmeng’enyo wa chakula tumboni, huongeza kunyonywa kwa chakula na kuzuia maumivu ya tumbo yanayosababishwa na ulaji wa chakula kingi.

Kadhalika, alisema husaidia kupunguza uvimbe wa viungo unaojulikana kama ‘rheumatoid arthritis’ na husaidia mapambano dhidi ya magonjwa yanayosababisha mtu kushindwa kupumua vizuri kama mafua na kikohozi.

Gedi alisema chai ya tangawizi ‘antioxidants’ zinasaidia kuboresha mfumo wa kinga mwilini na hivyo humsaidia mtumiaji kuondokana na hatari ya kupata kiharusi kwa kuzuia mafuta katika kuta za mishipa ya damu.

Alisema faida nyingine husaidia kupunguza au kutuliza msongo wa mawazo na pia husaidia kuondoa tatizo la kukosa choo.

“Inapunguza maumivu ya misuli, kuondoa uchovu, kupunguza uzito, kutoa gesi chafu tumboni, inaongeza hamu ya kula kwa kuchochea uzalishwaji wa acid (tindikali) za kumeng’enya chakula katika tumbo.

“Kwa wale wanaosumbuliwa na baridi yabisi unywaji wa chai ya tangawizi husaidia kuondokana na tatizo hilo,” alisema.

Gedi alisema vilevile kuwa, unywaji wa chai ya tangawizi husaidia kusafisha utumbo mkubwa, huponyesha maumivu ya misuli na pia kinywaji cha kiungo hicho kinaweza kutumiwa kama dawa ya kuchua.

Credit - Nipashe
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: