ads

KATIKA kile kinachoonekana ni lengo la kulinufaisha taifa na rasilimali zilizopo kama ilivyo katika nchi zingine ikiwamo Afrika Kusini (maarufu Sauzi), Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema nia ya chombo chake ni kuhakikisha kuwa umiliki wa hisa kwa nchi unafikia kiwango cha asilimia 16 hadi 50.


Vyanzo mbalimbali vinaonyesha kuwa katika mataifa yanayosifiwa kufanya vizuri kwenye kusimamia rasilimali zao barani Afrika, ikiwamo Afrika Kusini, yenye utajiri mkubwa wa dhahabu, umiliki wa hisa kwao huwa wa kiwango cha juu kama alichokitaja Ndugai.

Hivi karibuni, Afrika Kusini ilianza mchakato wa kuhakisha kuwa licha ya Serikali kuwa na hisa za kutosha, bado kunakuwapo na vipengele vya sheria vinavyolazimisha migodi yote kuwa na wamiliki weusi walio wazawa wa nchi hiyo kuwa na hisa zinazofikia asilimia 30, ikiwa ni nyongeza ya asilimia nne kutoka kiwango cha awali.

Akizungumza bungeni mjini Dodoma jana, Ndugai alisema miswada iliyowasilishwa bungeni kuhusu masuala ya madini itaboresha ushiriki na umiliki wa Watanzania kwenye madini na kuwa huo wa asilimia 16 hadi 50 kama ambavyo wamekuwa wakililia jambo hilo siku zote.

Ndugai alitoa ufafanuzi huo alipokuwa akitoa matangazo mbalimbali, hiyo ikiwa ni siku moja baada ya serikali kuwasilisha miswada mitatu inayohusiana na dhamira ya kuona kuwa taifa linanufaika na rasilimali zake zikiwamo za madini.

“Pamoja na mambo mengine, (miswada) inaboresha ushiriki na umiliki wa Watanzania katika masuala ya madini kwa kuanza kuwa na hisa asilimia 16 hadi 50… kama Bostwana na nchi nyingine,”alisema Ndugai.

Akifafanua, Spika alisema kuwa kamwe hawezi kutounga mkono uwasilishwaji wa miswada yenye tija kwa taifa kama hiyo, akipangua hoja za baadhi ya wabunge waliotilia shaka juu ya uwasilishwaji wa miswada hiyo kwa hati ya dharura.   

Alisema uzuri wa miswada hiyo pia ni pamoja na ukweli kuwa inapunguza nguvu ya waziri na Kamishna wa Madini katika masuala ya rasilimali za taifa kama za migodi ya madini.

“Maana hii nguvu ilileta shida, sasa zinapunguzwa… si mlikuwa mnapiga kelele fulani kafanya hivi mara nani kafanya hivi?”Alihoji Ndugai.

Kadhalika, Ndugai alisema kuna muswada utafanya uwepo wa makamishna watatu wa madini na maamuzi yao ya mikataba yatapelekwa kwenye Baraza la Mawaziri na kisha bungeni.

Miswada iliyowasilishwa na Serikali kwa hati ya dharura bungeni, na ambayo ilimlazimu Spika kuongeza siku tano zaidi ili ifanyiwe kazi ni kutungwa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili, 2017, ikiwamo kutaka kila Mtanzania kulinda na kusimamia kikamilifu rasilimali za Nchi kwa masilahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Muswada mwingine unakusudia kupendekeza kutungwa kwa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ambazo ni Sheria ya Madini, Sura ya 23, Sheria ya Petroli, Sura ya 392, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya  332, Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura ya 148 na Sheria ya Bima, Sura ya 394.

Aidha, muswada wa tatu unapendekeza kutungwa kwa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba inayohusu Maliasili za Nchi.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: