AKITUA tu nchini na kumalizana na Simba, mshambuliaji mwenye kasi na mwendo wa kuyumba uwanjani, Emmanuel Anorld Okwi ndiye atakuwa mchezaji ghali zaidi wa Simba.
Simba imejipanga kumalizana na Okwi kwa dau la dola 50,000 (Sh milioni 110), pia atakabidhiwa nyumba ya kuishi katika maeneo ya Sinza, Mbezi Beach au Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba, tayari kupitia kamati ya ufundi na ile ya usajili, wamekubaliana kuwa Okwi ndiye chaguo namba moja kwa wachezaji wa kigeni.
Juzi, Okwi aliliambia Championi kutoka Senegal kwamba bado hawajafanya mazungumzo “siriaz” na Simba, lakini wakikubaliana yuko tayari kuja.
Imeelezwa kwa kuwa Okwi yuko huru, yaani hana mkataba na Sports Club Villa anayoichezea, kamati hiyo imekuwa ikipambana kuhakikisha dau hilo linashuka angalau kufikia dola 25,000 (Sh milioni 55).
Kiongozi mwingine anayehusika na usajili alisema: “Fedha hizo ni nyingi sana, Okwi hana mkataba na Villa, hivyo najua itapungua ili kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. Simba tungependa kununua wachezaji kwa kupunguza gharama.”
Habari kutoka ndani ya Simba tayari wanahangaika kupata fedha hizo na tayari kiasi fulani kimepatikana tayari kumshusha Okwi Dar es Salaam.
“Kamati imepitisha na tumekubaliana, tunataka mtu wa kuamua matokeo timu inapokuwa imezidiwa. Tunataka mtu wa kushirikiana na wenzake kumaliza kazi na Okwi hatuna shida naye,” alisema.
Kama hiyo haitoshi, imeelezwa mmoja wa wanachama wenye nazo ndani ya Simba, yeye ameamua kutoa gari lake ili Okwi awe analitumia wakati akiwa Tanzania.
Mganda huyo yupo Senegal ambako timu ya taifa ya Uganda, The Cranes imeweka kambi na wikiendi hii inacheza dhidi ya Ivory Coast.
Baada ya hapo, Okwi atarejea Kampala na matumaini makubwa kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, dili litakuwa limefungwa na Okwi kutangazwa rasmi huku akirudishiwa jezi yake namba 25.
Credit - Champion
Post A Comment: