BAADA ya kikosi chake kufanikiwa kumaliza mwaka kikiwa kinaongoza
msimamo wa Ligi Kuu Bara Kocha mkuu wa Simba, Joseph Omog amesema sasa
ameanza kuona mwanga wa ubingwa.
Kikosi cha Simba juzi kilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Ruvu
na kuzidi kujichimbia kileleni ikiwa na pointi 41 dhidi ya 37 za
mabingwa watetezi Yanga walio katika nafasi ya pili.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Omog aliwapongeza
wachezaji wake kwa kucheza kwa kujituma ingawa alikiri mchezo ulikuwa
mgumu kwani wapinzani wao walionekana kuwakamia.
Simba itacheza na Ruvu Shooting Alhamisi ya wiki hii kabla ya kwenda
kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza Desemba 30.
Yanga itacheza na Ndanda.
“Nawapongeza sana wachezaji wangu walicheza vizuri muda wote wa
mchezo ingawa pia nawapongeza wapinzani wetu JKT Ruvu nao walicheza
vizuri na kutupa presha muda wote wa mchezo lakini mwisho wa siku
tulipata pointi tatu,”alisema Omog.
Alisema atahakikisha jitihada walizo nazo wanaziendeleza na kwenye
mechi zinazofuata ili kufanikiwa kutwaa ubingwa msimu huu kama
walivyokusudia.
Aidha Omog, alisema kitengo cha timu yao kuanza mwaka mpya wa 2017
wakiwa kileleni mwa msimamo wa ligi ni dalili njema kwao ingawa ndiyo
kwanza mzunguko wa pili umeanza lakini anafurahi kuona wachezaji wake
wanacheza kwa kujituma na kuonesha bidii katika kila mchezo.
Kocha huyo alisema atahakikisha wanafanya kila linalowezekana ili
kuendelea kupata matokeo katika mechi zao zinazofuata ili wabaki kwenye
nafasi hiyo ya kwanza hadi mwishoni mwa ligi hiyo kama ambavyo
wanapanga.
Alisema kitendo cha kuwaacha wapinzani wao Yanga kwa pointi nne ni
moja ya ishara ambazo za timu yake kuwa mabingwa msimu huu kwani kwa
kasi waliyokuwa nayo hafikirii kama wanaweza kuondoka kwenye nafasi
hiyo.
“Yanga wasijidanganye kwamba wanaweza kutuondoa kwenye nafasi hii ya
uongozi, kwa sababu tumekusudia kuwa mabingwa msimu huu maana tumewazidi
kwa kila kitu,” alitamba Omog.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI



Post A Comment: