KATIKA namna isiyotazamiwa kutokea kwenye
maeneo mengine nchini, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema na
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, wamevaana tena na kupigana
vijembe.
Kisa cha kuvaana tena kwa wawili hao, kinadaiwa kuwa siyo kingine
isipokuwa ni kutifautiana kwao mtazamo kuhusiana na namna ya kuongoza.
Lema anamtuhumu Gambo kuingilia baadhi ya mambo asiyostahili kwa nafasi
yake huku Gambo akisisitiza kuwa kamwe hawezi kuyumbishwa na mambo ya
kisiasa.
Tukio hilo ambalo ni mwendelezo wa jingine la aina hiyo lililotokea
siku tatu zilizopita, lilijiri juzi na kisha kujirudia tena jana wakati
wawili hao walipokutana kwenye vikao muhimu vya utendaji katika mkoa
wao.
Oktoba 18, wakati wa kuzindua ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto,
itakayojengwa kwa ufadhili wa taasisi ya Martenity Africa, Lema na Gambo
walishuhudiwa wakitunishiana misuli baada ya kutofautiana juu ya
historia ya mradi huo.
Jambo hilo lililozua gumzo kubwa, lilitokea wakati Gambo akijaribu
kuelezea historia ya kiwanja cha jengo hilo na Lema kumpinga kwa sauti
ya juu, akimshutumu kuwa anaupotosha umma kuhusu ukweli wa mradi huo;
hali iliyowalazimu polisi waliokuwapo kuingilia kati na kutuliza mambo.
Juzi, Lema na Gambo walikutana kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya
Mkoa (RCC) na kuonekana wakiendeleza malumbano yao kwa kurushiana
vijembe, kila mmoja kwa wakati wake akimlaumu mwenzake kwa mambo
mbalimbali.
Katika kikao hicho, Lema alikuwa akimlaumu Gambo kwa kuingilia baadhi
ya mambo ambayo aliyodai kuwa siyo yake kiutawala huku Gambo naye
akijibu mapigo kwa kusema hatakubali kuyumbishwa na mambo ya kisias
Katika kikao cha jana ambacho kilikuwa cha 38 cha Bodi ya Barabara,
wawili hao walikutana na kuketi kwa ukaribu zaidi tofauti na juzi baada
ya wajumbe wa mkutano huo kumchagua Lema kuwa makamu mwenyekiti huku
Gambo akiwa mwenyekiti.
Viongozi hao, ambao licha ya kukaa karibu, kwa muda mwingi
walionekana kutochangamkiana wala kuonyeshana sura za bashasha. Hata
hivyo, waliendesha vyema kikao hicho, licha ya kwamba Lema alionekana
akitoka kabla ya kufikia mwisho.
Haikujulikana mara moja chanzo cha Lema kuondoka kabla ya kikao
kufikia mwisho, ingawa wakati akiwamo kikaoni alitoa maoni yake kadhaa
ikiwa ni pamoja na kutaka taa ziwekwe kwenye eneo la kona ya Mbauda
jijini humo.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI



Post A Comment: