Mbunge wa Chambani, Yusuph Salum Hussein (CUF) jana alichafua hali ya
hewa bungeni baada ya kusema kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
lilitumika kupindua Mapinduzi ya Zanzibar katika uchaguzi wa marudio
uliofanyika Machi 20 mwaka huu visiwani humo.
Alikuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Wakati akichangia bajeti hiyo, Yusuph alisema jeshi limekuwa
likifanya kazi katika mazingira magumu lakini limetumika kupindua
Mapinduzi ya Zanzibar na limetengewa asilimia 18 katika bajeti ya
maendeleo.
Wakati anaendelea kuzunguma Spika wa Bunge, Job Ndugai alimwambia:”
Mheshimiwa Yusuph umetumia maneno ambayo yanatupa tabu, kwamba jeshi
limetumika kupindua Zanzibar…hebu liweke vizuri.”
Baada ya kauli hiyo ya Spika, Yusuph alijibu akisema:”Mheshimiwa
Spika Oktoba 25 mwaka jana kulikuwa kuna Uchaguzi Mkuu, wananchi wa
Zanzibar wakachagua chama chetu cha CUF lakini baadaye uamuzi ule
ukapinduliwa…naendelea ambaye hajaridhika anione nimsomeshe,”alisema
huku wabunge wa CCM wakizomea.
Alipomaliza kuchangia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenister Muhagama aliomba
mwongozo kwa Spika akitumia kanuni 68 (7)
“Maana ya mapinduzi wote tunafahamu na hasa katika uchaguzi, leo
tunapotoa taarifa kwamba jeshi ambalo hata mbunge anayechangia
amelisifia …anapokuja kulituhumu kwamba limefanya mapinduzi ni jambo
ambalo si kweli kabisa”.
Hapo Spika Ndugai alisimama akimwambia Yusuph kwamba amesikia maelezo ya waziri hivyo afute kauli yake.
“Mheshimiwa Spika sifuti kauli yangu kwa sababu ninao ushahidi wa
kila kituo kwamba chama chetu kilishinda na ninachokisema ninakiamini
ndani ya nafsi yangu,”alisema huku Spika akimwambia anampa nafasi ya
mwisho kufuta kauli hiyo na kwamba asilete habari ya vyama.
Hatimaye Yusuph alikubali kufuta kauli yake huku Spika akiwataka
watu wa hansard kufuta kauli hiyo ya jeshi kupindua Zanzibar na
lisionekane mahali popote.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: