WASAFIRISHAJI nchini wamempongeza Raisi John Magufuli kwa juhudi zake
zilizoiwezesha Tanzania kupata mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la
mafuta litakalojengwa kutoka Uganda hadi Tanga.
Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA) pia kimeipongeza timu
ya mazungumzo iliyoongozwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, huku kikiwataka wanachama wake na wadau wote kwa
ujumla kuchangamkia fursa nyingi na kubwa za kibiashara zitakazotokana
na ujenzi wa bomba hilo.
“Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa rais wetu na timu iliyoshiriki
kwenye mazungumzo, wametufanyia jambo kubwa katika ujenzi wa uchumi wa
nchi...imebaki juu yetu kupanga mikakati ya namna ya kutumia fursa za
kibiashara zitakazoletwa na mradi huu,” alisema Mwenyekiti wa Tatoa,
Angelina Ngalula jijini Dar es Salaam jana.
Ngalula alisema kutokana na fursa hii kubwa iliyopatikana, wadau wote
wa bandari wana wajibu wa kuitumia katika kutangaza bandari zilizopo
nchini ili kuvutia wawekezaji na wateja katika kukuza uchumi wa nchi.
“Fursa hii kubwa itaifanya Bandari ya Tanga kuingia katika ramani ya
dunia hivyo basi ni vyema wadau wote wa bandari na wapenda maendeleo
kuitumia vizuri nafasi hii,” alisema mwenyekiti na kuongeza kuwa
utekelezaji wa mradi huo wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,403 kutoka
Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga utatengeneza fursa nyingi za
usafirishaji mizigo kwa njia ya reli na barabara.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: