
BAJETI ya tatu ya serikali ya awamu ya tano inatarajiwa kuwa Sh. trilioni 32.476, imeelezwa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango ndiye alibainisha hilo alipokuwa akiwasilisha bungeni mjini hapa jana mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2018/19 na Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti kwa mwaka ujao wa fedha.
Alisema maoteo ya awali yanaonyesha kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 764 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka huu ya Sh. tril. 31.712.
Katika bajeti ya mwaka 2016/17 ambayo ilikuwa ya kwanza kupitishwa na bunge chini ya uongozi wa Rais John Magufuli, serikali iliidhinishiwa kutumia Sh. tril. 29.53.
Dk. Mpango alisema maoteo ya Sh. trilioni 32.476 kwa bajeti ya mwaka ujao wa fedha, yatathibitishwa baada ya kufanya uchambuzi wa mwenendo wa utekelezaji wa bajeti katika nusu ya kwanza ya mwaka 2017/18.
Alisema mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 22.088 (asilimia 68 ya mahitaji yote), mapato ya kodi yatakuwa Sh. trilioni 18.817 (asilimia 85.2 ya mapato ya ndani), mapato yasiyo kodi yatakuwa Sh. trilioni 2.424 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri yatakuwa Sh. bilioni 847.7.
MIKOPO
Waziri huyo alisema serikali inatarajia kukopa Dola za Marekani milioni 600 (Sh. trilioni 1.374) kutoka vyanzo vya nje yenye masharti ya kibiashara na mikopo ya ndani Sh. trilioni 4.029 kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zilizoiva.
Aidha, Dk. Mpango alisema Sh. trilioni 1.327, sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa, itakuwa ni mikopo mipya ya ndani kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh. trilioni 3.658 ambapo Sh. bilioni 946 ni misaada na mikopo nafuu ya kibajeti, Sh. trilioni 2.153 ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh. bilioni 558.9 ni misaada na mikopo nafuu ya mifuko ya pamoja ya kisekta.
MATUMIZI
Alisema serikali itatumia jumla ya Sh. bilioni 32.476 ambazo matumizi ya kawaida yatakuwa Sh. trilioni 20.228 na maendeleo Sh. trilioni 12.248.
Alisema kuwa kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Sh. trilioni 7.628 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi za umma na Sh. trilioni 9.705 ni kwa ajili ya Deni la Taifa.
Kwa upande wa matumizi ya fedha za maendeleo, Dk. Mpango alisema Sh. trilioni 9.536 (asilimia 76.6) ni fedha za ndani.
VIPAUMBELE
Alisema Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka ujao wa fedha utazingatia maeneo manne ya kipaumbele ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa miaka mitano.
Alisema kipaumbele cha kwanza ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kikilenga kuendelea kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hususani za kilimo, madini na gesi asilia.
Dk. Mpango alisema vipaumbele vingine ni kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu, ujenzi wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mpango kwa kuboresha ufuatiliaji, tathmini na utoaji taarifa za utekelezaji wa mpango.
Post A Comment: