MKE wa aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Kigoma Kusini David Kafulila, Jesca Kishoa amesema sababu alizozitoa mume wake kujiondoa kwenye chama hicho zinatumiwa na wanasiasa ambao hawana misimamo na wasio wapambanaji kujijengea uhalali wa kisiasa.


Hata hivyo, Kishoa ambaye ni Mbunge wa viti maalum(Chadema) amesisitiza kuwa yeye binafsi hatakihama chama hicho na ataendelea kuwa mwanasiasa makini bila kuyumbishwa na msimamo wa mume wake.

Kishoa aliyasema hayo jana katika ofisi za chama hicho kanda ya kati mjini hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimamo wake baada ya Kafulila kujiondoa Chadema.

Alisema kuwa sababu ambazo Kafulila amezitoa hazina mashiko kwani zimekuwa zikitumiwa na wanasiasa ambao hawana misimamo na sio wapambanaji katika kutetea misimamo yao.

Aidha alisema kuwa kwa vile anavyomfahamu Kafulila, hafikiri kuwa sababu hizo ndizo zilizomfanya ajitoe Chadema bali kuna nyingine ambayo yeye mwenyewe anaijua moyoni mwake.

“Mimi nilipata taarifa za Kafulila kujiondoa Chadema kama ambavyo watu wengine wamepata," alisema Kishoa. "Yeye akiwa Dar es Saalam na mimi nipo Dodoma na hajanishirikisha kwa lolote juu ya uamuzi wake huu aliouchukua.”

Kafulila alijiondoa katika chama hicho juzi na kudai kuwa upinzani kwa ujumla umepoteza ajenda ya vita ya ufisadi na kumsifia Rais John Magufuli kuwa ndiye mpambanaji kwa sasa.

Lakini Kishoa alisema jambo hilo siyo la kweli kwani upinzani ndiyo ambao umekuwa ukifichua masuala hayo.

“Nyote mnafahamu jinsi ambavyo Chadema imekuwa ndani ya agenda ya ufisadi," alisema kwa sababu "tumezungumzia Lugumi, ununuzi wa ndege ambao haukufuata utaratibu, mabehewa hewa na kuibua mambo mengine makubwa ikiwa pamoja na sakata la Escrow."

"CCM sio sehemu sahihi ya kupambana na ufisadi hata yeye Kafulila anajua hilo.”

Alisema yeye hayumbishwi na chochote kutokana na kuhama kwa mumewe na kwamba ataendelea kuwa mwanasiasa makini wa Chadema.

“Alichokifanya Kafulila ni haki yake kikatiba na mimi siwezi kabisa kuyumbishwa na msimamo wake.

"Ninao uhakika kuwa kuna sababu nyingine ambazo zimemfanya afikie maamuzi haya kwani toka nimekuwa naye sikuwahi kumuona akiisifia CCM bali alisimamia misimamo yake.”

Kafulila alifunga pingu za maisha na Jesca Novemba 23, 2014.

Juzi Kafulila alitangaza kukihama chama hicho kwa madai kuwa upinzani umepoteza dira ya vita ya ufisadi.

Alisema kwa kipindi kirefu amekuwa Mbunge pekee aliyesimamia ajenda ya ufisadi bungeni kitendo ambacho kimempa tuzo na heshima ndani na nje ya nchi.

Kafulila alisema hatua anazochukua Rais Magufuli wapinzani wamepigwa ganzi na ameona hakuna mwelekeo wowote ndani ya upinzani wa kupambana na ufisadi.

ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: