ads

WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, amewakaribisha kujiunga na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wanachama waliokatwa majina yao katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Aboubakary Lyongo jana ilimkariri Lowassa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, akiwataka makada hao wa CCM wahamie upinzani ambako "watafurahia demokrasia".

"Nimesoma na kusikia baadhi ya waliokuwa viongozi CCM wamekatwa ama kutetea nafasi zao au kugombea kwa sababu mbalimbali na jina langu limekuwa likiendelea kutajwa tajwa humo," ilimkariri Lowassa taarifa hiyo na kumnukuu zaidi:

"Mimi nawaambia hawa Watanzania wenzetu waliokatwa huko CCM nawakaribisha huku Ukawa (Chadema) wafurahie demokrasia."
Lowassa aligombea urais kwa tiketi ya Ukawa, mwamvuli wa kisiasa uliounganisha mbali na Chadema, vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kushindwa na John Magufuli wa CCM.

Lowassa ambaye alipata kura milioni 6.072, sawa na asilimia 39.9, alisema Chadema na upinzani kwa ujumla kuna maisha mazuri ya kisiasa hivyo wasisite kujiunga.

Aidha, taarifa hiyo ilisema Lowassa amekumbusha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema ni wakati mwafaka kwa Tanzania kuwa na mfumo wa vyama vingi.

"Nataka kuwakumbusha Watanzania wenzangu hawa, uamuzi ule wa Baba wa Taifa ulilenga kuwapa Watanzania demokrasia ya kuwa na uwanja mpana wa kufanya siasa," ilimkariri taarifa hiyo.

"Mimi nimetumia fikra hizo za Mwalimu na hakika hivi sasa ninafurahia demokrasia halisi huku niliko."

Taarifa ilisema aliwaambia wote waliokatwa na kuhisi kuwa wameonewa, waondokane na unyonge wa fikra kudhani kuwa bila CCM hakuna maisha na badala yake wahamie upinzani.

Aidha, Lowassa aliwaomba wanachama wenzake wa Chadema kuwapokea kwa mikono miwili wana CCM watakaojiunga nao sasa, taarifa ilisema na kueleza zaidi kuwa amewataka wanaoendelea kubaki chama tawala kuendelee kushikamana hadi Uchaguzi Mkuu ujao 2020.

CCM haijawahi kutamka hadharani hata hivyo kukata mwanachama wake yeyote katika ngazi yoyote ya uongozi kwa sababu ya kuwa na uhusiana na Lowassa, licha ya madai hayo kuenezwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, aliwaambia waandishi wa habari Jumamosi iliyopita kuwa kikao cha Halmashauri Kuu Taifa ya Chama cha Mapinduzi (NEC), kilipitisha majina 161 kati ya 1,400 walioomba kugombea uenyekiti ngazi ya Wilaya.

Alisema uchaguzi wa Wilaya sita ulifutwa baada ya kubainika kuwa walioshinda hawakuwa na sifa za kimaadili.

Alisema Wilaya za CCM ni zile za kiserikali, hivyo kikao kimefanya uteuzi huo na kimeridhia kwa kauli moja huku akifafanua kuwa nafasi kwenye Wilaya ambazo uchaguzi umefutwa zitatangazwa upya.

Alizitaja Wilaya hizo kuwa ni Moshi Mjini, Siha, Hai, Musoma Mjini, Musoma Vijijini na Makete na kwamba CCM ilijiridhisha wagombea waliojitokeza walikuwa na kasoro nyingi za kimaadili na kikanuni
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: