ALIYEKUWA daktari wa familia ya msanii wa filamu, Stephen Kanumba, Dk. Paplas Kagaiga (35), amedai mahakamani katika kesi inayomkabili Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, kuwa alipompima msanii huyo nyumbani kwake alikuwa ameshakufa.


Kadhalika, amedai kuwa alipompima Kanumba mapigo ya moyo yalikuwa yamesimama hayafanyi kazi na kwamba alimshauri mdogo wa marehemu, Seth Bosco, kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili ili daktari mwingine akathibitishe. 

Kagaiga alitoa ushahidi  huo jana mbele ya Jaji Sam Rumanyika anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam. 

Upande wa Jamhuri uliongozwa na jopo la Mawakili wa Serikali, Faraja George, Yusuph Aboud na Batlida Mushi huku ile wa utetezi ukiwa na mawakili Peter Kibatala na Omary Msemo.

Akiongozwa na Wakili Mushi, shahidi alidai kuwa Aprili 7, 2012 saa 6:00 usiku akiwa ofisini kwake, Manzese, Dar es Salaam alipigiwa simu na Bosco aende nyumbani kwao Sinza huku akimweleza kuwa Kanumba ameanguka.

"Nilimjibu usiku ule hakuna usafiri akanieleza ananifuata na gari... kwa sababu mimi nilikuwa daktari wa familia yao, nilitayarisha vifaa vya matibabu mara alifika tukaenda," alidai.

Aliongeza kuwa: "Nilipofika nilimkuta Kanumba amelala chali sakafuni, nilimpima sukari ilikuwa kawaida, nilipompima mapigo ya moyo yalikuwa yamesimama hayafanyi kazi... Nilimshauri Bosco tumpeleke Muhimbili akafanyiwe vipimo vikubwa. Tulipofika
kitengo cha dharura daktari alithibitisha kuwa amefariki dunia."

Baada ya hapo, alidai kuwa alikwenda kituo cha polisi Salender Bridge kuchukua fomu namba tatu, akiwa ameongozana na askari watatu kwenda Muhimbili kuhifadhi mwili.

Alidai kuwa wakati wa uhai wake, Kanumba alikuwa anapata matibabu kwenye hospitali yake na alimtibu maradhi mbalimbali ikiwamo malaria na mengine ya kawaida na kwamba alifahamiana na Lulu kwa sababu alikuwa mpenzi wa Kanumba.

Naye shahidi wa tatu,  Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP)  Ester Zephania (47), kutoka kituo cha polisi Msimbazi,  alidai kuwa siku ya tukio akiwa katika kituo chake cha kazi Oysterbay, aliitwa na bosi wake aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Cammilius Wambura (kwa sasa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum Dar es Salaam (ZCO) na kumwagiza kwenda Sinza nyumbani kwa Kanumba kukagua tukio.

Alidai kuwa aliongozana na askari waliokuwa zamu maarufu Kama Kiboko 42 pamoja na Msanii wa filamu, Vincent Kigosi, maarufu kama Ray hadi nyumbani kwa Kanumba.

Alidai kuwa alipofika nyumbani kwa Kanumba alikuta watu wengi, wengine walikuwa wakilia kuonyesha mazingira ya msiba na alijitambulisha kwa watu hao kuwa yeye ni askari.

"Wenyeji waliniitia Bosco nikamwuliza kilichojiri, akanielekeza chumbani kwa Kanumba... Nilikuta kitanda kimevurugika, juu ya stuli kulikuwa na chupa ya β€˜whisky’ aina ya Jack Daniels na glass, chini ya kitanda niliona mpini wa panga."

"Ukutani kulikuwa na mmburuzo uliokuwa na rangi nyeusi, nilimpigia simu Afande Wambura kumjulisha yaliyotokea akanieleza atatuma timu ya ukaguzi wa matukio maarufu kama Nyota 333. walipofika nilijiondoa eneo la tukio ili waendelee na majukumu yao," alidai.

Pia alidai kuwa bosi wake alimpa jukumu lingine la kumpata Lulu.

" Nikiwa na wafuasi wangu tulimtumia Dk. Kagaiga kumkamata Lulu alimvuta hadi Bamaga Sinza tukamkamata," alidai ASP Zephania.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Aprili 7, 2012 eneo la Sinza Vatican, Dar es Salaam, mshtakiwa alimuua Kanumba bila kukusudia. Mshtakiwa alipokumbushwa shtaka lake jana alikana.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: