ads

Mkusanyiko wowote ambao unatarajiwa kufanyika kumuombea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, utakumbana na wakati mgumu kutoka vyombo vya dola.


Polisi imeshazuia mkusanyiko wa maombezi hayo uliokuwa umeandaliwa na Chadema mjini Sumbawanga kwa madai kwamba utasababisha uvunjifu wa amani.

Jana, Baraza la Vijana Chadema (Bavicha) lilitangaza kufanya maombi kama hayo ya Sumbawanga kesho jijini Dar es Salaam huku likiwaalika viongozi mbalimbali wa dini lakini kabla siku yenyewe haijafika, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa ameyazuia na kutangaza kutoruhusu mkusanyiko wowote wenye nia ya kumuombea mtu fulani.

Awali, Bavicha ilisisitiza kwamba haitarajii kuona maombi hayo yakizuiliwa kwa sababu hawaendi kufanya siasa, bali maombi kwa ajili ya Lissu na viongozi wengine wa Taifa kama ambavyo wamekuwa wakitoa wito wa kuombewa.

Maombi ya Bavicha yamepangwa kufanyika katika viwanja vya TIP, Sinza na tayari viongozi mbalimbali wa Kiislamu na Kikristo wamealikwa kwa ajili ya kuongoza maombi hayo.

Makamu Mwenyekiti wa Bavicha (Tanzania Bara), Patrick Ole Sosopi aliwaambia wanahabari jana katika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam kuwa, “Sisi tumeratibu tu maombi haya lakini hatutazungunza chochote, tutawaacha viongozi wa dini waongoze maombi hayo.”

Ole Sosopi alisema wametuma barua ya mwaliko kwa taasisi mbalimbali za dini ikiwamo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na kwamba wanasubiri majibu.

“Tumetoa taarifa pia kwa jeshi la polisi kama sheria inavyotaka. Hatutarajii kuzuiwa kwa sababu tumefuata taratibu zote kama sheria inavyotaka. Mmiliki wa uwanja amekubali, Serikali ya mtaa pia imeridhia jambo hilo,” alisema Ole Sosopi na kusisitiza “Hili jambo ni la kitaifa, tutalifanya kwa amani na utulivu mkubwa.”

Alisema ikitokea kuzuiwa, jeshi la polisi litoe sababu za msingi kwa nini wanawanyima wananchi haki yao ya kufanya maombi.

“Viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwamo Rais John Magufuli wamekuwa wakiwataka wananchi wawaombee, nasi katika maombi haya tutakwenda kumwombea ndugu yetu Lissu pamoja na viongozi wengine kwa ujumla,” alisema Ole Sosopi.

Ni kama Ole Sosopi alikuwa anajua kile ambacho kingefuata kwani baadaye Kamanda Mambosasa aliitisha mkutano na wanahabari akisema suala la maombi halijanza leo wala jana hivyo wakazi wa kanda maalumu (Dar es Salaam) lazima wafuate utaratibu.

“Hivi mtu anatoka Kimara, mwingine Mwenge halafu mnakutana sehemu kisha mnakwenda kufanya maombi Msimbazi! Haya hayatakuwa maombi, bali maandamano na hatutayaruhusu na wakithubutu kufanya hawatazidi hatua tano, wataangukia mikononi mwa polisi,” alisema.

“Ukiwa kanisani wewe fanya maombi hata usiku kuchwa hatutashughulika na wewe.”

Kamanda Mambosasa alisema maombi yanafanyika katika sehemu maalumu lakini kitendo cha watu kujikusanya sehemu moja kisha kuanza safari ya kwenda kufanya maombi mahali fulani siyo sahihi na ni kutotii sheria zilizopo.

Ndugai ataka Lissu aombewe, wabunge wachukue tahadhari

Wakati polisi na Bavicha wakivutana kuhusu maombi hayo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka wabunge kuendelea kumuombea Lissu na wale watakaopata nafasi ya kwenda kumuona jijini Nairobi wampelekee ujumbe.

Sambamba na kumuombea mwenzao ambaye alishambuliwa kwa risasi zinazodaiwa kuwa ni zaidi ya tano akiwa kwenye gari nje ya nyumba yake Alhamisi iliyopita mjini Dodoma, Spika aliwatahadharisha wabunge kuhusu usalama wao.

Akizungumza muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa Bunge jana, Ndugai aliwataka wabunge kuwa makini popote wanapokwenda kutokana na kuwapo kwa matukio mengi ya uhalifu nchini.

Aliwataka wasikae sana katika baa, “Yaani tuchukue hatua tu katika maisha yetu kama mnavyosikia matukio ni mengi katika nchi yetu. Usalama unaanza na wewe mwenyewe kwanza.”

Alisema vyombo vya usalama vinavyowalinda, vinaongezea kidogo na kuwataka kutazama nyendo zao za namna wanavyoishi.

“Kwa wale tuliozoea saa saba (usiku) ndiyo tunarudi nyumbani basi tuanze kurudi mapema kidogo. Lakini pia tuangalie usalama wa familia zetu na tuwaambie wapigakura, naona siku hizi watoto wanapotea, watoto wanauawa,” alisema.

Aliwataka wabunge kuwapelekea huo ujumbe wananchi kuwa wawe makini na watoto wao wakati wa kwenda shule na maeneo mengine kwa kuhakikisha wanajua mtu anayewapeleka na kuwachukua.

“Hayo mambo yanayofanana na hayo. Ushauri ni wa ujumla tu,” alisema.

ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: