WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Charles Tizeba, sasa ameibukia kuboresha zao la kahawa ikiwa siku chache baada ya kukwepa kutumbuliwa na Rais John Magufuli.
Tizeba alinusurika kuingia katika mtego huo wa kufungishwa virago baada ya kutekeleza agizo la Rais la kumtaka ahakikishe amekipatia hati kiwanda cha kusindika maziwa cha Tanga Fresh.
Baada ya kukwepa mtego huo, Dk. Tizeba ameapa kuifumua Sheria ya Bunge iliyounda Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kwa madai kuwa ndiyo suluhu ya kwanza kunusuru zao hilo.
Amesema sheria hiyo haiwasaidii wakulima wala taifa na badala yake imelikwepa jukumu la msingi la usimamizi wa uzalishaji na kulisukumia kwa halmashauri na wadau.
Akiwa katika makao makuu ya bodi hiyo mjini hapa jana, aliagiza Mshauri wa Sheria wa TCB, Engisaria Mongi, kufunga safari ya kwenda wizarani kwa ajili ya kuanza marekebisho ya sheria.
Wakati akiagiza kufumuliwa kwa sheria hiyo, Dk. Tizeba pia aliwatahadharisha wafanyakazi wa TCB wajiandae kubadilishiwa majukumu yao na watakuwa wanajihusisha na maendeleo ya kahawa.
“Inaonekana suala la uzalishaji wa kahawa halina mwenyewe. Kuna haja ya Bunge kuifumua sheria iliyounda Bodi ya Kahawa nchini, lazima tuirejeshee TCB jukumu lake la kwanza la msingi ambalo ni kuhakikisha inasimamia na kuendeleza kahawa nchini,” alisema.
Tanzania inauza kahawa yake kwenye soko la dunia kila mwaka karibu tani 50,000 zinazolimwa katika hekta zisizopungua 230.
Licha ya udhaifu huo wa kisheria, ambao alidai kuwa tatizo linalolitumbukiza shimoni zao hilo na kuwafanya wakulima kung’oa mibuni na kupanda mazao mengine mbadala, Waziri Tizeba alisema inashangaza kwa sababu hata suala la mbolea na viuatilifu halizungumzwi na wataalamu wake na halina changamoto kama yalivyo mazao mengine kama pamba na korosho.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Primus Kimaryo, alimweleza Waziri Tizeba kuwa TCB ni taasisi ya serikali iliyopewa jukumu la kusimamia maendeleo ya kahawa nchini kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na. 23 ya mwaka 2001 na mabadiliko yake ya Sheria ya Mazao Namba 9 ya Mwaka 2009.
UTOROSHAJI KAHAWA
Akiwa katika bodi hiyo, Waziri Tizeba alihoji kuhusu udhibiti wa usafirishaji wa kahawa ya magendo kwenda nje ya nchi, unaofanywa na wafanyabiashara wa zao hilo kupitia maeneo ya Kyaka, Karagwe na mpaka wa Kanyigo.
"Hawa wafanyabiashara wanaotorosha kahawa yetu kwenda nje ya nchi wametupiga vya kutosha, nyie kama bodi mmegundua nini," alihoji.
Baada ya swali hilo, Kimaryo alisema walichokigundua katika maeneo hayo ni kuwa baadhi ya wanunuzi wa kimataifa hasa kutoka Uganda, ambao hufanya biashara na vyama viwili vya ushirika vya Karagwe (KDCU) na Kagera (KCU0 hutumia mbinu ya kutopitisha kahawa yao viwandani na kutumia kitu kinachoitwa ‘Mobile Halas’ yaani benki zinazohama kununua na kusafirisha kwa magendo.
Maeneo yanayolalamikiwa kukithiri kwa biashara hiyo ya magendo ya kahawa ni Kanyigo, Bandari bubu ya Mwaru iliyoko mkoani Kagera, Kyaka na Karagwe.



Post A Comment: