BAADA ya vipimo vya mkojo kuonyesha kuwa na chembechembe za dawa za kulevya aina ya heroin, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema mfanyabiashara Yusufally Manji, anayekabiliwa na mashtaka ya kutumia dawa za kulevya, ana kesi ya kujibu.
Wakati mahakama ikimwona Manji ana kesi ya kujibu, upande wa utetezi ukiongozwa na Hudson Ndusyepo, umedai kuwa unatarajia kuita mashahidi 15 kupangua tuhuma dhidi ya Jamhuri.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha, baada ya kusikiliza mashahidi watatu wa upande wa mashtaka.
Alisema mahakama yake baada ya kupitia ushahidi wa Jamhuri uliotolewa na mashahidi watatu bila kuacha shaka, imemwona Manji ana kesi ya kujibu.
"Mshtakiwa mahakama hii imekuona una kesi ya kujibu na itaanza kusikiliza ushahidi wa utetezi Agosti 30 na 31, mwaka huu," alisema Hakimu Mkeha.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu eneo la Upanga Sea View, jijini Dar es Salaam, Manji alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin.
Katika ushahidi uliotolewa, shahidi wa tatu katika kesi hiyo, mkemia Domician Dominic (42), alidai mahakamani Jumanne wiki hii kwamba alipima mkojo wa Manji mara mbili.
Dominic alidai kuwa alipopima sampuli ya mkojo wa mfanyabiashara huyo kwa mara ya kwanza, alikuta una chembechembe za dawa zinazotumika kutuliza maumivu makali na za usingizi.
Kadhalika, alidai kuwa vipimo vya awamu ya pili vilionyesha chembechembe za dawa zinazotokana na dawa za kulevya aina ya heroin.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitals, shahidi huyo wa Jamhuri alidai kuwa alifanya vipimo hivyo baada ya kupokea sampuli ya mkojo wa mshtakiwa aliyefikishwa ofisini kwake akiwa chini ya ulinzi wa Koplo Sospeter.
Alidai kuwa alipoipima sampuli hiyo kwa awamu ya kwanza alibaini kuwapo kwa kundi la dawa za 'Benzodiezepines',
chembechembe ya dawa mbalimbali zinazotumiwa na watu wenye maumivu makali na zinazosababisha usingizi ambazo zinatolewa kwa maelekezo maalumu ya madaktari.
Alidai kuwa katika awamu ya pili ya vipimo vya sampuli hiyo, alibaini 'Metabolities', chembechembe za dawa zenye heroin ambazo zina matumizi sawa na zile za awamu ya kwanza.



Post A Comment: