ads

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema idadi ya watalii wanaoingia nchini kila mwaka ni ndogo kulinganisha na vivutio vilivyopo, hivyo kuitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kutafuta mbinu bora za kujitangaza, ili kukuza sekta hiyo.


Waziri Mkuu aliyasema hayo jana alipofanya ziara katika mji wa kitalii wa Varadero ulioko kwenye mkoa wa Matanzas, nchini Cuba.

Katika taarifa iliyopatikana jana jijini Dar es Salaam, alisema mji wa Varadero tu unaingiza zaidi ya watalii milioni moja kwa mwaka na unategemea kivutio kikubwa kimoja tu cha ufukwe ambao una urefu wa kilomita 22.

Alisema idadi hiyo ni tofauti na Tanzania ambayo imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii huku watalii wanaovitembelea ni wachache na kusema: “Tunatakiwa kujitangaza zaidi.”

Waziri Mkuu alitaja baadhi ya vivutio vya utalii ambavyo ni Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, miji ya kihistoria ya Kilwa, Bagamoyo (Pwani), Stone Town (Zanzibar) na Mikindani (Mtwara).

“Vivutio vingine ni eneo la Oldvai George ambako binadamu wa kwanza aliwahi kuishi, hifadhi ya Gombe ambako kuna sokwe ambao wanaishi kama binadamu,” alisema.

Ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na tija, alisema Serikali itahakikisha jitihada zinafanyika katika kukuza utalii ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vilivyoko nchini, ili kuongeza idadi ya watalii.

Pia Waziri Mkuu aliwahamasisha Watanzania kujenga tabia ya kutembelea vivutio vya utalii na kujifunza mambo mbalimbali na si kuwaachia wageni pekee.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Sekta ya Utalii katika mkoa wa Matanzas, Luis Martinez de Armas, alisema mji wa Varadero ni kivutio kikubwa cha utalii nchini Cuba.

Alisema kivutio kingine cha utalii ni hoteli zilizojengwa ndani ya bahari, maeneo ya kihistoria na migahawa inayouza vyakula vya asili vya nchi hiyo.

Luis alisema mwaka 1990 walianza kuendeleza sekta ya utalii katika mkoa wao na ulikuwa na hoteli 4,436 ambazo kwa sasa zimeongeza na kufikia 20,696.

Hata hivyo, Luis alisema Tanzania inavivutio vingi vya utalii na kwamba anavutiwa na Mlima Kilimanjaro pamoja na wanyama na viumbe vingine vilivyoko katika mbuga mbalimbali.

Alisema wako tayari kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya utalii.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: