ads

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara (2017/18) unatarajiwa kuanza leo kwa michezo saba kufanyika kwenye viwanja tofauti hapa nchini kuanza mbio za kumsaka bingwa mpya.


Mabingwa wa Kombe la FA, Simba wao watashuka kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuumana na Ruvu Shooting kutoka Pwani.

Simba inaingia uwanjani leo huku ikiwa bado kwenye furaha ya ushindi wa matuta 5-4 walioupata dhidi ya watani zao Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliofanyika Jumatano iliyopita.

Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog akizungumza na gazeti hili jana, alisema kuwa kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo.

“Baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii tumefanya mazoezi juzi na jana, hakuna shaka yoyote, wachezaji wapo vizuri na wanajua umuhimu wa ushindi kwenye mchezo huu wa kwanza,” alisema Omog.

Mbali na mchezo wa leo wa Simba dhidi ya Ruvu Shooting, michezo mingine ya leo itashuhudia Mbao watawakabili Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Majimaji ya Songea itakayosafiri hadi Mbeya kucheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine wakati Njombe Mji itaialika Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sabasaba huko Makambako.

Aidha kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro, wenyeji Mtibwa Sugar wataikaribisha Stand United ya Shinyanga wakati Azam FC itaumana na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Mwadui FC ya Shinyanga watakuwa wenyeji wa Singida United.

Ligi hiyo inatarajia kuendelea kesho kwa mashabiki wa Yanga kufaidi tena mambo ya kiungo wao mpya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, KabambaTshishimbi wakati watakapowakaribisha wageni wa ligi hiyo Lipuli ya Iringa ambayo inanolewa na kiungo wa zamani wa Simba, Selemani Matola.

Wakati huo huo Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema kuwa shirikisho hilo linasisitiza kuwa Ligi Kuu ifanyike kwa uadilifu ili kupata mwakilishi bora wa nchi katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika ya mwaka 2019.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: