Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikishirikiana na Wizara ya Fedha, imesambaza maafisa wake katika halmashauri 169 kote nchini ili kutoa mafunzo katika vituo vyote vya makusanyo ya kodi jinsi ya kukusanya kodi kwa simu ya mkononi.
Zaidi ya maafisa 170 kutoka makao makuu ya Wizara ya Ardhi, Wizara ya Fedha na kutoka kanda nane za ardhi wameanza kutoa elimu hiyo katika halmashauri na vituo vyote vya makusanyo ya kodi ya ardhi ili kurahisisha ulipaji kodi ya ardhi kwa wananchi kwa kutumia simu zao na kuondoa usumbufu.
Mfumo wa ulipaji kodi ya pango la ardhi kwa njia ya simu ya mkononi ni mfumo wa kielektroniki wa Government electronic Payment Gateway (GePG) katika makusanyo ya kodi ya pango la ardhi ambao utamrahisishia mwananchi kulipia popote walipo kwa kutumia simu zao kwa urahisi zaidi.
Mwananchi yeyote anayemiliki kiwanja au shamba lililopimwa na kupatiwa hati, ataweza kutumia simu yake ya mkononi kujua kiasi cha kodi ya pango la ardhi anachodaiwa na kukulipa kwa kutumia simu yake ya mkononi.



Post A Comment: