ads

TAHARUKI ya aina yake iliwakumba abiria waliokuwamo ndani ya basi la lililogonga treni jana, mjini Morogoro na kusababisha vifo vya watu watatu na kuwajeruhi vibaya wengine 28.


Aidha, ilidaiwa kuwa dereva wa basi hilo, lililokuwa limejaza wanafunzi wa shule mbili za sekondari alichangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa maafa hayo baada ya kupuuza tahadhari aliyopewa na hivyo kujikuta akipokea kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira kabla ya kulazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Morogoro akiwa taabani.

Undani wa chanzo cha ajali hiyo, uliwekwa wazi na mmoja wa majeruhi aliyeisimulia Nipashe hali ilivyokuwa sekunde chache kabla ya ajali hiyo iliyotokea majira ya asubuhi.

Ajali hiyo, ilihusisha basi lililokuwa limebeba wanafunzi wa shule mbili za sekondari waliokuwa wakielekea shuleni, ambalo liliigonga treni ya abiria.

Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei alisema ajali hiyo, ilitokea saa moja asubuhi katika eneo la Tanesco, kwenye makutano ya Reli ya Kati na barabara.

Alisema ajali hiyo, ilihusisha daladala lenye namba za usajili T438 ABR aina ya Toyota Coaster linalofanya safari zake za Kihonda-Mjini.

Alisema basi hilo la abiria 28 lilikuwa limebeba wanafunzi wa shule za sekondari za Tushikamane na Mjimpya, zote za kata ya Kihonda, Manispaa ya Morogoro.

Akizungumzia ajali hiyo, mmoja wa majeruhi waliokuwa katika basi hilo, Rukia Selemani ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili sekondari ya Tushikamane, alisema walimpigia kelele dereva kuhusu ujio wa treni, lakini aliwaambia wasimfundishe kazi.

"Tulimpigia kelele sana dereva kuhusu kitambaa chekundu chenye kumzuia, lakini alijaribu kuyapita magari mengine na kabla ya kuvuka reli tukasikia kishindo kikubwa," alisema Selemani.

Baadhi ya mashuhuda walimvamia dereva wa gari hilo, na kumshushia kipigo kutokana na kusababisha ajali hiyo, alisema mwanafunzi huyo. Dereva huyo amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kufuatia kipigo hicho cha wananchi.

Kamanda Matei alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Coaster ambaye licha ya kuonyeshwa kitambaa chekundu akisimamishwa asipite, alilazimisha kuyapita magari yaliyokuwa yamesimama mbele yake na kukutana na treni hiyo ya abiria iliyokuwa karibu na kuigonga.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Frank Jacob alisema alipokea majeruhi wa ajali hiyo, hospitalini hapo na kwamba kati yao, wanafunzi watatu walifariki wakati wakipatiwa matibabu.

Aidha, ilielezwa kuwa Polisi ililazimika kutumia nguvu kwa baadhi ya wazazi na ndugu na jamaa za wanafunzi hao waliofika katika hospitali hiyo kujua hali za abiria wa basi hilo.

Mmoja wa wazazi aliyejitambulisha kwa jina la Zubeda Hassan alisema, utaratibu mbaya hospitalini hapo uliwazuia kuingia hivyo kupelekea wazazi, ndugu na jamaa kufanya vurugu kwa kurusha mawe getini kushinikiza lifunguliwe.

Credit - Nipashe

ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: