Baada ya jeshi la polisi kumkamata Tundu Lissu siku ya Alhamsi uwanja wa ndege akiwa anaelekea nchini Rwanda. Jana jeshi hilo lilikwenda kufanya upekuzi nyumbani kwa Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.
Siku ya jana Ijumaa ya tarehe 21/07/2017 jeshi la polisi walimchukua Tundu Lissu na kwenda naye mpaka kwa Mkemia Mkuu wakiwa na lengo la kutaka kumpima mkojo kabla ya kuelekea nyumbani kwake kufanya ukaguzi. Lakini kiongozi huyo aligoma kufanya kipimo hicho kwa madai kuwa tuhuma anazotuhumiwa haziendani na vipimo hivyo.
Kwa mujibu wa Tumaini Makene ambaye ni Afisa habari wa (CHADEMA) anasema kuwa jana polisi baada ya kufanya ukaguzi nyumbani kwa Tundu Lissu waliweza kuchukua CD 6 na kuondoka nazo.
"Jeshi la Polisi bado linamshikilia, Mhe. Tundu Lissu, Kwenye upekuzi jana nyumbani kwake walichukua CD 6 za 1996 zinazohusu masuala ya mgodi wa Bulyag'hulu, Shinyanga" ilisema taarifa ya CHADEMA .
Leo ni siku ya pili toka kiongozi huyo anashikiliwa na jeshi la polisi Dar es Salaam lakini Wakili Peter Kibatala pamoja na Wakili Fatma Karume wa IMMA Advocates kwa upande wao wanasema wanaendelea na juhudi za kisheria kuhakikisha kiongozi huyo anapatiwa dhamana au kufikishwa mahakamani mapema iwezekanavyo.
Post A Comment: