ads

KASI ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) katika kutekeleza majukumu yake kwenye siku za hivi karibuni, iliendelea kudhihirika juzi wakati uchunguzi wao ulipoiwezesha mahakama kumtia hatiani mmoja wa vigogo wa nafasi za juu katika kampuni binafsi.


Aliyekutwa na hatia katika kesi hiyo iliyokuwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, ni Mkurugenzi Mtendaji na mmiliki wa Kampuni ya Mpasunka General Supplies and Contractors, Deusdedit Kisisiwe. Mshtakiwa alihukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya Sh. milioni 5.5.

Aidha, kigogo huyo alitakiwa kulipa kila senti aliyotuhumiwa kuifuja, hiyo ikiwa ni matokeo ya amri ya mahakama ya kumtaka alipe fedha zote kiasi cha dola za Marekani 888,900 (zaidi ya Sh. bilioni 1.6) alizokutwa na hatia ya kuzifuja, ambazo ni za kampuni ya MEIS Industries.

Taarifa iliyotolewa jana na Takukuru kuelezea hukumu hiyo ya Julai 25, 2017, mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Wilbard Mashauri, ilieleza kuwa adhabu ilitolewa baada ya mahakama kuridhika pasi na shaka na ushahidi wa upande wa mashtaka ulioongozwa na waendesha Mashtaka wa Takukuru, Magela Ndimbo na Godliver Kilia.

Ilielezwa zaidi kuwa kesi hiyo ya aina yake kwa Mkurugenzi Mtendaji na Mmiliki wa kampuni binafsi kushtakiwa na kupatikana na hatia ya kosa la rushwa, ilifunguliwa na Takukuru Oktoba 21, 2014; na Kisisiwe alishtakiwa kwa mujibu wa kifungu namba 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Awali upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa katika tarehe tofauti, kati ya Julai 25, 2011 na Novemba 20, 2012, katika maeneo yasiyofahamika jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mpasunka, alifanya ufujaji wa fedha hizo (dola za Marekani 888,900), ambazo alikuwa amekabidhiwa na Kampuni ya MEIS Industries.

Aidha, ilielezwa kuwa kabla ya mahakama kutoa hukumu yake, wakili wa Serikali, Emmanuel Jacob, aliyemwakilisha mwendesha mashtaka wa Takukuru, Magela Ndimbo, aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na watu wengine wanaofikiria kufanya ubadhirifu wa mali waliyokabidhiwa na wengine.

Aidha, wakili Jacob aliiomba mahakama imwamuru mshtakiwa arejeshe dola 888,900 alizofuja kwa mujibu wa kifungu cha 28(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Kabla ya hukumu, wakili wa kujitegemea aliyekuwa akimtetea mshtakiwa, aliiomba mahakama imwonee huruma na impunguzie adhabu mshtakiwa kwa kuwa mbali ya kufanyiwa upasuaji wa moyo, pia ana familia kubwa inayomtegemea.

Kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, ndipo mahakama ilipomtia hatiani Kisisiwe kwa kumhukumu kulipa faini ya Sh. milioni 5.5 au kwenda jela pamoja na kurejesha fedha zote dola 888,900 alizofuja kwa MEIS.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari na Uhusiano na Takukuru, Mussa Misalaba, hadi juzi jioni wakati muda wa kazi ukimalizika mahakamani hapo, mshtakiwa alikuwa bado hajalipa faini ili aepukane na kifungo.

Hivi karibuni, Takukuru iliendelea kudhihirisha makucha yake katika kutibua tuhuma mbalimbali za ‘dili’ za upigaji baada ya kuwafikisha watu kadhaa kortini kwa makosa yanayohusiana na rushwa, utakatishaji fedha na pia uhujumu uchumi.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: