UMOJA wa madhehebu ya Kikristo mkoani Dodoma umesema utaandaa siku maalum ya kumpongeza na kumuombea Rais John Magufuli kutokana na kazi anazofanya zinazoleta tumaini jipya kwa wananchi wa kawaida.
Mwenyekiti wa umoja huo, Dk Damas Mukasa alisema hayo juzi kwenye makao makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo wanachama, wazee wa mkoa wa Dodoma na viongozi wa chama ngazi ya mkoa na wilaya ya Dodoma Mjini walipojitokeza kumpongeza Rais Magufuli kutokana uamuzi mgumu anaochukua wa kulinda rasilimali za nchi.
Dk Mukasa alisema kazi anazofanya Rais Magufuli zinaleta msisimko kwa wananchi wa kawaida hasa kwa kubaini ufisadi mkubwa kwenye raslimali za nchi. “Anaondoa mafisadi anahakikisha rasilimali za nchi hazinufaishi watu wachache, ameondoa watu wasiostahili serikalini, tumeona kwa macho yetu na kushuhudia alivyoiondoa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA),” alisema.
Alisema hata mwanzoni mwa wiki hii, Rais Magufuli alipotoa ripoti kuhusu ufisadi mkubwa unaofanyika kwenye madini wananchi wameshangilia. “Wakristo wa Dodoma wamefurahishwa sana na uamuzi huo tutaandaa ibada maalumu ya kumpongeza Rais Magufuli kwa uamuzi mgumu anaochukua wa kulinda maslahi ya nchi kwa manufaa ya taifa,” alisema.
Kwa upande wake kada wa CCM, Emmanuel Kamara alisema ripoti ya pili kuhusu madini rais Magufuli ameipokea kwa weledi na upeo mkubwa. “Rais alichogundua waliotuangusha ni ni watanzania wenzetu tena ni wasomi ni viongozi wetu na tena na cha kusikitisha zaidi walifanya kama makusudi katika kutekeleza jambo hilo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CCM, mkoa wa Dodoma Balozi Job Lusinde alisema sasa ni wakati wa kuunga mkono juhudi za Rais ili nchi ikae kwenye mstari. Katibu wa baraza la wazee mkoa wa Dodoma, Mohamed Makbel alisema watanzania wana kila sababu ya kumshukuru Mungu kutokana na madudu yanayoibuliwa ambayo yalifanya taifa lipate hasara kubwa kutokana na tamaa za watu wachache.
Post A Comment: