MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari amemfananisha Rais John Magufuli na Rais wa Kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah na Waziri Mkuu wa Kwanza wa Congo (DRC), Patrice Lumumba kutokana na juhudi binafsi anazofanya kutetea rasilimali za nchi.
Wakati Profesa Safari akisema hayo, Mbunge wa Chambani, Yusuf Salim Hussein (CUF) amesema anamuunga mkono Rais Magufuli, kwani amejitoa mhanga kwa maslahi ya taifa. Aliwaambia wabunge vita hiyo ni ngumu na wanapaswa kumshukuru Rais bila ya kujali kama ni wa CCM, Chadema au CUF.
“Sisi si maadui, tuungane tuwe pamoja kwa maslahi ya taifa, tujiulize tunataka kwenda wapi, tusameheane na twende mbele kwani tukipasuka hatutafika,” alisema. Kwa upande wake, Profesa Safari alisema hayo ofisini kwake Dar es Salaam jana, alipotoa maoni yake juu ya agizo la Rais kutaka iundwe timu ya wataalamu kupitia upya sheria za madini nchini na kupelekwa bungeni ili zifanyiwe marekebisho.
“Ninampongeza Rais John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kutetea rasilimali za nchi. Anafanya kazi kama walivyokuwa wanafanya baadhi ya viongozi wazalendo barani Afrika ya kupigania haki za wananchi wao kufaidika na rasilimali za nchi,” alisema Profesa.
Alitoa mfano wa Patrice Lumumba, Kwame Nkrumah na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kama viongozi waliojitolea kwa ajili ya wananchi wao. Alisema maamuzi anayoyafanya Rais yanasimama katika Kifungu cha Tisa (Kifungu Kidogo C) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho ya mwaka 2000, ambacho kinasisitiza kwamba utajiri wa Taifa uendelezwe, uhifadhiwe na kutumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine.
Profesa Safari aliwaomba Watanzania na wataalamu wa sheria za mikataba, kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais katika kutetea maslahi ya Taifa. “Nchi hii ina wanasheria wengi wazuri katika masuala ya madini na mikataba. Ninashauri watafutwe wataalamu hawa watakaokuwa sio wala rushwa ili wamsaidie Rais katika vita hii ya rasilimali,” aliongeza Profesa Safari.
Akizungumza kwa niaba ya wazee waliofika Ikulu kusikiliza ripoti ya Kamati ya pili ya kuchunguza mchanga wenye madini, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alielezea ujasiri unaofanywa na Rais Magufuli kuwa ni mfano wa kuigwa na Watanzania kuunga mkono juhudi za Rais kutetea rasilimali.
Post A Comment: