SIMBA ni miongoni mwa wanyama ambao ni jamii ya paka, ukiondolea mbali kwamba ndiye mnyama mkubwa anayewinda katika jamii yao hiyo, lakini pia ni wanyama ambao hupenda kuishi kwa makundi makundi. Kwa lugha nyingine naweza kusema wanaishi kifamilia kama ilivyo kwa binadamu na familia zao huweza kuwa na simba takribani kumi na watano.
Njia rahisi ya kuwatambua kwa jinsia zao ni muonekano pamoja na majukumu, wakati simba dume shingoni likiwa limejaa manyoya mengi, simba jike huwa na manyoya sawa mwili mzima, hapo ni kwa mtazamo wa namna wanavyoonekana.
Katika majukumu, simba hugawana kazi ya kuhakikisha chakula cha kutosha kinapatikana katika familia, hilo ni jukumu la simba jike na simba jike aendapo mawindoni jukumu la simba dume ni kulinda mipaka tu. Uzito wa mnyama huyu huwa kati ya kilo 120 mpaka 240 inategemea na umri pamoja na afya.
Uhai wa simba kuishi ni kati ya miaka 10 mpaka 14 lakini kwa simba wa Afrika hufika hadi miaka 17 na zaidi. Simba huanza kufundisha mbinu za uwindaji watoto wake tangu wakiwa wadogo kabisa, ambapo huwatanguliza mbele na kuanza kuwabughuzi kwa kuwapiga piga ngwala, jambo ambalo hufanya watoto wake kuwa wenye hasira na wakali sana na mbinu hizo ndio hutumia akiwa anawinda ukubwani.
Simba mara zote hupendelea kukaa sehemu ambazo kuna miamba mizuri, pamoja na nyasi kavu kavu ambazo hufanana kwa mbali na rangi yake, kwakuwa huishi kifamilia dume ndio huanzisha makazi mapya, ambapo likiunguruma kwa sauti yake, sauti hiyo husafiri umbali mrefu na sehemu inayoishia ndio huwa mpaka wa makazi yao na kama katikati ya sauti hiyo itakumbana na makazi ya simba wengine, basi dume jingine litaitikia, hapo kinachofuata ni simba hao kuhama lakini kama hawatakubaliana kutoka basi madume ya pande hizo mbili yatakutana kuoneshana ubabe na litakalokubali kushindwa litaondoka na familia yake.
Simba dume huchukia sana jike akizaa dume, hasira yake huja pindi anapoyafikiria madaraka, kwani hutambua jamaa hao ndio watakao kuja kumpindua ili wao ndio wawe watawala, hivyo chuki yake hukuwa kila watoto hao wanapozidi kuongezeka kimo. Jukumu kubwa la kuyalinda madume hayo huwa chini ya mama yao, siku akizembea tu simba dume huvinyonga kikatili, mtifuano huo huwa hauishii kwa watoto tu. Hata simba dume linapozeeka na kushindwa kutimiza majukumu yake kwa ustadi hufukuzwa kabisa na wanafamilia wenza na nafasi yake itachukuliwa na simba dume ambaye anachipukia kwa wakati huo.
Kwa jina la kisayansi simba huitwa Pantela Leo, kuna msemo usemao akikosa nyama basi hula majani, msemo huu si sahihi inapotokea simba anakula majani si sababu ya njaa, bali hutumia baadhi ya mimea hasa majani, kama tiba pindi anaposumbuliwa na ugonjwa hususani tumbo.
Pamoja na kutumia tiba hiyo, lakini pia wana tabia ya kunyanyapaa simba mwenzao hasa anapopata ugonjwa ambao huonekana ni hatarishi katika jamii yao, badala ya msaada wenzie huamua kumtenga na kumfukuza ili kuepuka ugonjwa huo kusambaa zaidi.
Post A Comment: