KURUGENZI ya Ulinzi ya Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Prof Ibrahim Lipumba
Imedai itazuia ziara za Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ambazo amepanga kufanya Dar es Salaam, ikiwa hataishirikisha kurugenzi hiyo kwa ajili ya ulinzi.
Kurugenzi hiyo imetoa tamko hilo siku chache baada ya Maalim Seif kusema anakusudia kufanya ziara wakati wowote mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Kurugenzi hiyo Bara, Athuman Hamad, alidai kwa mujibu wa katiba ya CUF, kiongozi yeyote wa chama hicho anapofanya mikutano lazima alindwe na walinzi wa chama.
Alidai wameapa kukilinda chama na wako tayari kumlinda Maalim Seif katika ziara zake, lakini anatakiwa afuate utaratibu kwa kupitia ofisi za chama na kuwashirikisha walinzi wa chama.
Alisema ni vema Maalim Self akaondoa hofu na kufika katika ofisi hizo kwa ajili ya kuendelea na shughuli zake kama kawaida na wao wako tayari kumlinda kama wanavyofanya kwa viongozi wengine.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama Bara, Masoud Omari, alidai chama chao hakiendeshwi kiholela, hivyo hawawezi kumruhusu Maalim Seif na kama atafanye ziara bila ya walinzi wa chama.
Nipashe lilipomuuliza Ofisa Habari na Mawasiliano wa chama hicho Zanzibar, Hissham Abdukadir, alisema ziara za Maalim Seif zitafanyika kama zitakavyopangwa na kamati husika kwa mujibu na taratibu za chama na hakuna wa kuzuia.
Alisema ratiba ya ziara za Maalim Seif Bara inatarajiwa kutolewa wakati wowote baada ya kumalizika kwa tathmini ya ziara zake alizozifanya Kisiwani Zanzibar.
“Ratiba ya ziara za Katibu Mkuu zilipangwa kufanyika Bara baada ya kumalizika kwa ziara zake alizokuwa anazifanya upande wa Zanzibar, ambazo zilimalizika jana (juzi), kwa hiyo kinachofanyika kwa sasa ni tathmini na baada ya hapo itatolewa ratiba ya ziara zake wakati wowote kwa upande wa Bara na zitafanyika kama zitakavyopangwa,” alisema Abdulkadir.
Post A Comment: