KABLA ya ujio wa kundi lao ambalo ndani ya kipindi cha miaka minne mfululizo walijenga imani ya mashabiki kwao kama Bendi yenye vijana wenye vipaji ambao wana uwezo wa kutoa ngoma kali, tayari yeye alishakuwepo.
Alikuwepo kabla hata ya wenzake kuhisi ipo siku watatoka kimuziki, alishajenga jina lake kabla mwenzake yule wa Kigamboni hajapanda Pantoni na wale wengine wawili hawajatua Ubungo wakitokea mikoani, Aslay alishakuwepo.
Unapozungumzia mastaa ambao walifanikiwa kutoka haraka na kukamata nyoyo za mashabiki katika umri mdogo, Aslay hawezi kukosekana.
Eeh kama utataja listi ya waliotoka angali wadogo kiumri basi utamueka pamoja na Mr Blue, Dogo Janja na labda Young Dee.
Aslay alisikika akiwa mdogo hata Elimu ya Msingi akiwa hajamaliza, siyo tu kusikika bali kuwa Staa ambaye wimbo wake wa Naenda Kusema ukigeuka kuwa wimbo wa Taifa.
Yaani upo Shule ya Msingi wimbo wako unageuka kuwa wimbo wa Taifa.
Haikua bahati bali uwezo ambao umekuwepo ndani yake, haikuja hivi hivi bali ilikuwa alama ya ustaa ambao taa yake iliwaka akiwa bado mdogo.
Siyo Maromboso, Enock wala Beka ambaye alikuwepo wakati Aslay anaachia naenda kusema, kabla ya kuja kutumaliza na niwe nawe aliompa shavu Mh Temba.
Kuna watu walizaliwa kuwa mastaa, kuna ambao wametengezwa kuwa mastaa na wengine wameutafuta ustaa na ukatii kwao.
Aslay yupo katika kundi la kwanza, ustaa upo ndani yake ni yeye wa kuamua kuuachia uondoke, au aushikilie na awe staa mkubwa zaidi, awe Supastaa!
YA MOTO IMESAFISHA NJIA
Baada ya kuachia Niwe na wewe akiwa na Temba jina lake likapotea kwenye ramani ya muziki kwa muda huku ikielezwa kuwa ni ubize wake na Shule, na kwamba akimaliza atakuja rasmi kuiteka Bongo Fleva.
Kuundwa kwa kundi la Ya Moto Bendi ambalo lilikuwa chini ya Said Fella katika project ya Mkubwa na Wanawe kukamrudisha tena katika game Aslay.
Lakini sasa hakua peke yake, aliambatana na wenzie watatu ambao wakati anatamba na Naenda Kusema wao walikuwa bado hawajatoka, Beka, Maromboso na Enock Bella.
Ya Moto iliwaeka katika kilele kizuri vijana, waliachia ngoma kadri walivyoweza huku wakipata dili kibao za matamasha lakini bado haikuonekana kama wanakua kimuziki, kwanini? Twende taratibu.
Kwanza staili yao ya kuachia ngoma baada ya ngoma haikua afya njema kwa muziki wao, muda mwingine masikio ya shabiki yanachoka kukusikiliza kila muda yanatamani kusikia fleva nyingine, ‘why’ wewe kila siku tu utoe nyimbo?
Hata wasanii wakubwa Diamond, Vanessa Mdee na Ali Kiba hujipa muda wa kutamba mbele ya mashabiki hawatoi ngoma kila siku, eti kwa sababu una jina ndio uachie kila siku, biashara ya muziki haipo hivyo.
Lakini kwa upande wa pili ilikuwa faida kwa Aslay na wenzake, Aslay yeye alizidi kukuza jina lake kutoka pale alipokua ameishia baada ya wimbo wake wa mwisho wa Niwe na Wewe huku wenzake watatu wakifaidika na majina yao kumea kwenye game.
Ya Moto imefungua njia kwao imejenga majina yao na sasa wamekuwa mastaa kila kona ya Nchi hii, wamefanikiwa.
TURUDI NJIA KUU
Baada ya kuchepuka kidogo na kuiongelea Ya Moto sasa turudi kuzungumza na Aslay, kama ni kweli anahitaji kuboresha ustaa wake kama nilivyodokeza hapo juu.
Yeye tayari ni Staa nachoamini alizaliwa kuwa hivyo lakini ana uwezo wa kuboresha zaidi ustaa wake au auondoe kabisa na arudi kuwa mtu wa kawaida, yote yapo mikononi mwake. Tutajadili.
Ni muda sasa Ya Moto haipo kwenye ubora wake, haitoi rekodi zikapasua kwenye ngoma ya masikio ya mashabiki, mara ya mwisho kutoa hit ilikuwa mwaka jana mwanzoni na rekodi yao ya Mama.
Baada ya hapo sikumbuki tena kama wamewahi kuachia chuma kikali, walitoka na Rugby lakini ngoma ikabaki ya kawaida, na juzi tena nasikia wametambulisha mpya nayo haijaleta matokeo chanya, imegoma kupenya kama zile za awali.
Nje ya Bendi Aslay ni msanii ambaye anaweza kufanikiwa kama akiamua kuwekeza kweli na kuwa seriazi na kipaiji chake, uwezo wa kuimba peke yake ‘solo artist’ na akafanikiwa anao tuliona kabla ya Ya Moto na sasa Kidawa imetudhihirishie.
Anachopaswa kufanya ni kuamua kufanya kazi zake tofauti na familia yake ya Ya Moto, yaani atoke kama Solo, zungumza na Viongozi wako naamini ni watu makini watakuelewa kisha uangalie maisha yako nje ya Bendi.
Afya yako kimuziki itazidi kuimarika kama utaamua kutoka Solo lakini ndani ya Bendi sioni mafanikio yako binafsi, ni ngumu sana kufanikiwa kwenye makundi, Chege, FA, AY, wote walifanikiwa baada ya kutoka na kufanya kazi kama Solo.
Naamini akili yako kuna kitu inataka ndio maana umetoa nyimbo mbili, tatu zako mwenyewe, ni jambo zuri lakini lifanye kwa mapana na userious wa hali ya juu.
Unaweza kutafuta meneja nje ya Mkubwa na Wanawe.
Sio kwa maana mbaya lakini katika kukuza afya yako kimuziki, wewe ni staa mkubwa kama utaamua, umri wako upo katika wakati sahihi wa kung’aa.
Iamini akili yako, kiamini kilichopo ndani ya Ubongo wako!
Post A Comment: