
MBUNGE wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), ameibuka na kudai hakutekwa siku ya uchaguzi mdogo wa madiwani Novemba 26, mwaka huu, kama ilivyodaiwa na watu wengi.
Alisema, siku hiyo alikamatwa na polisi pamoja na mawakala aliokuwa nao.
Akizungumza na gazeti la Nipashe jana mjini hapa alisema, hakutekwa kama wananchi wengine walivyokuwa wanadai mitaani na katika mitandao ya kijamii, bali alichukuliwa na polisi kwenda kituo cha polisi Usa River.
Alisema hatua hiyo ilitokana na wao kuhoji kwa nini mawakala wa Chadema wametolewa nje ya vituo vya kupigia kura.
Alisema alikuwa msimamizi wa kata ya Leguruki iliyopo Arumeru ambayo ilikuwa inafanya uchaguzi wa diwani lakini akadai kilichofanyika kilikuwa ni dhuluma na siyo uchaguzi wa kidemokrasia.
“Kwa kweli kwa yale yaliyofanyika Arumeru hakuna demokrasia tena nchini, kwa hali ya kawada na ikibidi mheshimiwa Rais alete tu mswaada bungeni kufuta mfumo wa vyama vingi uliopo,’’ alisema.
“Mfano mtu wa kwanza alipokuwa anaingia kituo cha kupigia kura kama pale Leguruki alikuta sanduku la kura zimeishafika nusu na alipouliza aliambiwa toka nje wakati alikuwa hajawekewa hata mhuri kiganjani,’’ alieleza.
Aidha, alisema kitu kilichowatia hofu wananchi kuwa amevamiwa mbunge huyo ni kuona anachukuliwa na polisi pamoja na mawakala wa Chadema.
Alisema iliwachukua muda mrefu kufika kituoni hapo kwa kuwa mmoja wa mawakala aliyekamatwa nao alipata mshutuko na kuanza kutapika na hivyo walianza kumpeleka kituo cha afya ili apate matibabu.
Alisema kilichofanyika Arumeru ni ubakaji wa demokrasia na kwa kuwa mawakala walipewa barua kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wakaapishwa na watendaji wa kata lakini mkurugenzi alikuja kuwageuka na kuamua kuwabadilisha vituo majira ya saa sita mchana huku kura zikiendelea kupigwa.
Alisema wananchi waliposikia wamekamatwa waliacha kwenda kupiga kura hivyo kati ya watu 4,000 waliojiandikisha kupiga kura waliopiga kura ni kama 1,000.
“Sisi tulipokamatwa tuliteswa na maaskari kwa kutumwagia maji ya kuwasha machoni kuanzia mchana hadi usiku matokeo yalipotangazwa mpaka sasa macho yangu hayaoni vizuri,” alisema.
Akizungumzia wimbi la wabunge wa upinzani kuhamia CCM, alisema wanaofanya hivyo hawana msimamo na hawajielewi bali wanaangalia maslahi yao binafsi na ndio maana wanawasaliti wananchi waliowachagua.
Alisema wabunge wa namna hiyo hawafai kuwa wanasiasa kwa sababu hawajui wanachokifanya na wanaposema wanamuunga mkono Rais ni unafiki mtupu siyo kwamba inatoka moyoni mwao hali hiyo.
“Watanzania siyo wa kweli kwa mioyo yao hao wanaoamua kwenda huko kuacha vyama vyao hasa wabunge siyo wanaipenda CCM bali wana hofu na ndio maana wanaamua kumuunga mkono adui lakini wengi wao wana njaa,’’ alisisitiza.
Alisema wabunge wanaoamua kutimukia CCM ni wale waliokuwa wanatumiwa na chama hicho.
Alisikitishwa na wabunge vigeugeu ambao alisema hawaelewi kwa kuwa wanafiki kwa kudai wanamuunga mkono Rais wakati wanaona hali ya uchumi ni mbaya huku akidai wametoka kuambiwa kwenye vikao kuwa fedha iliyopo kwenye mzunguko ni Sh. bilioni 12 kutoka Sh. bilioni 200.
Hata hivyo, alishauri wabunge wa namna hiyo kuombewa kwa kuwa hawajui wanachokifanya na akasema watamuungaje mkono Rais wakati wanaona fedha nyingine inayotumiwa na serikali inakuwa haijatengwa na bunge hivyo anaona hakuna sababu ya kumuunga mkono Rais.
Post A Comment: