RAIS John Magufuli jana alimtangaza Prof. Frolens Luoga kuwa Gavana mteule wa Benki Kuu (BoT) wakati Prof Benno Ndulu akijiandaa kustaafu ndani ya miezi miwili ijayo, kwa mujibu wa sheria.


Rais Magufuli alisema ingawa alikuwa hajazungumza na Prof. Luoga kuhusu uteuzi huo, lakini Profesa huyo wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ndiye atakuwa Gavana mpya wa BoT.

Mtaalamu huyo wa sheria za kodi anakuwa gavana wa saba wa BoT tangu uhuru mwaka 1961 na maprofesa wa uchumi wamebainisha vigingi sita ambavyo mteule huyo anapaswa kujiandaa kuvikabili katika kuiongoza taasisi hiyo nyeti.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutunuku vyeti vya pongezi na shukrani kwa wajumbe wa Kamati Maalumu za Uchunguzi na Majadiliano kuhusu rasilimali za madini nchini, Rais Magufuli alisema amemteua Prof. Luoga kutokana na kazi nzuri aliyoifanya akiwa katika kamati ya majadiliano baina ya serikali na kampuni ya Barick Gold.

"Kwa kazi nzuri iliyofanywa na kamati hii ya makinikia, nimeamua kumteua Prof. Luoga kuwa Gavana mpya wa Benki Kuu baada ya gavana aliyekuwapo kubakiza siku chache kumaliza muda wake," alisema Rais Magufuli.

"Na kwa kuwa nimeshazungumza, gavana aliyekuwapo atafanya haraka haraka kumkabidhi majukumu gavana mpya."

Alisema Prof. Luoga ni mtaalamu wa masuala ya sheria ya kodi, hivyo watu wanaofungua akaunti za fedha nje ya nchi mwisho wao umefika.

Alisema wakati anafanya uteuzi huo, hakumweleza Prof. Luoga kama atamteua kuwa gavana mpya, lakini kwa kuwa imeshatokea "inabidi akubaliane na uteuzi".

VIGINGI SITA
Baada ya kutangazwa kwa uteuzi huo, gazeti la Nipashe lilizungumza na wataalamu wa uchumi ambao walibainisha changamoto sita ambazo Gavana mpya wa BoT huyo anapaswa kujipanga kuzikabili ili uongozi wake uwe na tija kwa taifa.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Humprey Moshi, alisema kigingi cha kwanza kinachomkabili Prof. Luoga BoT ni utekelezaji wa Sheria ya Utakatishaji Fedha kwa kudhibiti na kusimamia maduka ya kubadilisha fedha.

Alisema maduka hayo kwa muda mrefu yamekuwa yakiendeshwa kiholela bila usimamizi mzuri wa BoT.

Alisema kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha kila duka linakuwa sehemu ya benki ya biashara na lisiwapo hata moja linalojiendesha bila kufungamanishwa na benki.

"Wakati mwingine unaweza kwenda unataka Dola za Marekani 10,000 unapewa kirahisi tu, wakati kwa nchi nyingine unaambiwa hatuwezi kukupa zaidi ya Dola 6,000," alisema, "China huwezi kubadili zaidi ya dola 10,000 kwa siku, lakini kwa hapa kwetu unaweza kupewa kirahisi."

Prof. Moshi alisema ni lazima BoT ifahamu kiasi cha Dola kilichopo kwenye mzunguko, akitolea mfano wa nchi ya Malawi ambayo haina viwanda wala madini bali mazao ya biashara ya tumbaku na chai lakini sasa inabadili Dola moja kwa Kwacha 700 wakati nchini Dola moja inabadilishwa kwa Sh. 2,230 licha ya Tanzania kuwa na madini na rasilimali nyingine nyingi ikiwamo gesi na mafuta.

Mtaalamu huyo wa uchumi alisema kama siyo jitihada za Rais Magufuli kuzuia watumishi wa umma kusafiri kwenda ughaibuni, kulikuwa na uwezekano mkubwa Dola moja kubadilishwa kwa Sh. 4,000 hadi 5,000 mwaka huu.

"Ni lazima gavana ajue fedha zinazoingia na kutoka nchini ili kuweza kudhibiti mambo mbalimbali," alisema.

Prof. Moshi alisema Gavana mpya wa BoT anapaswa kudhibiti matumizi ya Dola nchini, akizitolea mfano nchi zenye uchumi imara kama vile Afrika Kusini ambayo haziruhusu matumizi ya Dola nchini mwake.

"Mfano mwingine tuna jirani zetu Kenya, Shilingi yao imeendelea kuimarika tofauti na yetu kwa kuwa wamedhibiti kwa kiasi kikubwa matumizi ya Dola nchini mwao, ukitaka kununua au kuuza unatumia Shilingi yao, lakini kwetu unatumia Dola kama kawaida," alisema.

Hoja hiyo ya Prof. Moshi iliungwa mkono na Profesa mwingine wa UDSM, Razack Lokina, alisema matumizi ya Dola kwenye bei ya bidhaa madukani au kwenye nyumba za kupanga ni changamoto kubwa kwa kuwa wengi huwa na viwango vyao vya kubadili fedha na siyo vilivyopo kwenye soko.

"Leo nikipewa nafasi ya kumshauri Prof. Luoga, nitamwambia afuatilie kwa makini wale wanaouza bidhaa kwa kutumia Dola na wanamtaka mnunuzi kulipa kwa fedha ya Kitanzania lakini kwa viwango vyao vya kubadili Dola na siyo vilivyopo sokoni," alisema mtaalamu huyo wa uchumi.

KUNUNUA DHAHABU
Prof. Moshi pia alisema kuwa ili kulinda sarafu ya Tanzania ni lazima BoT ianze utaratibu wa kununua dhahabu, almasi na tanzanite huku akidai kuwa mikataba mingi iliyoingiwa na nchi miaka ya 1990 bei ya madini hayo ilikuwa kwa kipimo kimoja cha Dola za Marekani 2,080 lakini sasa ni Dola 1,700.

"Iwapo madini yangenunuliwa wakati huo na kuuzwa sasa ni wazi kuwa nchi ingepata faida na sarafu yetu ingeimarika," alisema.
Msomi huyo alipongeza jitihada za serikali kuzibana kampuni kubwa za nje na kueleza kuwa kuna ujanja mwingi ambao lazima udhibitiwe kikamilifu.

"Mafanikio yote na suala la makinikia inaonyesha kwa kiasi gani ukihusisha wasomi wako wa ndani ambao ni wazalendo utapata kitu kizuri zaidi," alisema na kufafanua zaidi:

"Wakati wa kusaini mikataba ni vyema kuwapo jopo la watu wa nje na ndani ya serikali ili kuhakikisha inaleta faida kwa pande zote. Hii inaitwa 'win win'."

Mtaalamu mwingine wa uchumi chuoni hapo, Prof. Haji Semboja, alisema kigingi kigingine kwa Gavana mpya wa BoT ni umakini wa kuendana na mabadiliko yoyote ya kimfumo ndani ya taasisi hiyo ambayo yanaweza kuathiri mfumo wa uendeshaji wa Benki Kuu duniani.

Alisema BoT ni taasisi nyeti, hivyo Gavana wake anatakiwa kuangalia sheria inayotengeneza benki na kazi zake.

Alisema ana imani na Prof. Luoga kwa kuwa ni mwanasheria aliyesoma sheria za kiuchumi, hivyo atatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

"Akiona pana haja ya kubadili mfumo ahakikishe mfumo atakaopigania ni mzuri kweli kuliko ambao ameukuta, asitengeneze cha kuharibu kuliko kinachotengeneza," alisema.

MAENEO MENGINE
Prof. Semboja alisema Prof. Luoga anapaswa kuhakikisha mabadiliko yoyote atakayofanya yasiathiri uchumi na ajue ni mfumo wa kidunia kwa Benki Kuu kushirikiana, hivyo akiharibu ajue ataharibu na nyingine maeneo mengine duniani.

Mchumi huyo alisema changamoto nyingine kwa Prof. Luoga ni kuhakikisha sekta binafsi inahusishwa ipasavyo katika ujenzi wa uchumi wa nchi na kuwe na mizani sawa baina ya serikali na sekta hiyo kwa kuwa "hakuna ubishi kuwa sekta binafsi ni injini ya uchumi wa nchi".

Prof, Semboja pia alisema ni vyema Gavana mpya wa BoT akaishauri vyema serikali katika mabadiliko ya uchumi wa sasa kwenda kwenye uchumi wa viwanda ili ijiimarishe katika maeneo hayo.

Msomi huyo pia aliunga na Prof. Moshi kumshauri Pro. Luoga kuhakikisha madini yanakuwapo BoT.

"Pamoja na kupewa majukumu ya kuhakikisha sekta ya madini inapewa kipaumbele, kwa sasa inatakiwa madini yawapo BoT, jambo ambalo linahitaji matayarisho mazuri," alisema.

Prof. Semboja pia alisema Gavana mpya anapaswa kuhakikisha Tanzania inaaminika katika kusaidia sekta binafsi ili kuinusuru kukimbiwa na wawekezaji wa nje.

"Ili tufikie lengo la kuwa nchi ya maendeleo ya viwanda, BoT iweze kukaa na serikali ili sekta binafsi iwezeshwe kuwa sehemu ya maendeleo hayo," alisema.

Mbali na Prof. Ndulu (2008-2017), magavana wengine waliowahi kuongoza BoT ni Edwin Mtei (1966-1974), Charles Nyirabu (1974-1989), Gilman Rutihinda (1989-1993), Dk. Idris Rashid (1993-1998) na Dk. Daudi Balali (1998-2008).

Akizungumza muda mfupi baada ya uteuzi huo, Prof. Luoga alisema pindi atakapoanza kazi BoT, atajifunza masuala yaliyopo katika taasisi hiyo kwa kushirikiana na watendaji waliopo kwa kuwa hakuandaliwa kuwa gavana.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: