
Maelfu ya raia katika mji mkuu wa
Mali Bamako wanaendelea kufurika ili kujionea kile kilichotajwa kuwa
muujiza wa kidini katika ukuta mmoja ambao ulionekana wikiendi iliopita.
Wengi
wanaamini picha hiyo nyeupe katika ukuta wa nje wa choo inamuonyesha
mtu akisali na kuonekana kama ishara ya ujumbe wa Mungu.Maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia walipelekwa katika eneo hilo ili kudhibiti umati huo kwa kuwa watu wanapiga foleni usiku kucha kuona muujiza huo wa alama.
''Tunaamini ni maono ya mtume wetu'', Aliou Traore ambaye anaishi katika eneo hilo aliiambia BBC.
Bwana Traore amesema kuwa alama hiyo imekuwa ikibadilika tangu ionekane mara ya kwanza.''Mara nyengine alama hiyo inajifuta na kuonekana katika maeneo mengine ya nyumba hizi.Baadaye inarudi'',alisema.
Mwandishi wa BBC Alex Duval Smith mjini Bamako anasema kuwa watu hawalipi chochote kuona alama hiyo lakini wanawacha fedha katika ndoo,ambazo familia ya Traore inasema itazitoa kwa msikiti wa eneo hilo.
Wakati ripota wetu alipotembelea eneo hilo,alama hiyo ilionekana kama kovu la simiti la mwanamke aliyesimama.Picha za alama hiyo zimesambaa mjini Bamako kupitia simu tangu ionekane siku ya jumamosi.
Wafuasi wa Tijani ambao hupatikana magharibi mwa Afrika wanajulikana kwa kuheshimu miujiza.
Post A Comment: