
KAMA ulikuwa unaichukulia poa Yanga pole yako, ni kwa sababu pale Jangwani kwa sasa kumenoga kinoma.
Yanga inayohaha kuukarabati Uwanja wa Kaunda ili kuondokana na kujitia hasara ya kujitakia, kwa sasa ipo katika mstari na Katibu Mkuu wake Boniface Mkwasa amekiri bado kidogo tizi litaanza kupigwa Jangwani.
Mkwasa alisema makundi 68 ya Yanga ya mitandao ya kijamii ya Facebook na Whatsapp, yamechangia kiasi cha fedha za kutosha mpaka sasa kwa ajili ya maandalizi ya ukarabati wa uwanja wao.
“Niweke wazi kwamba tumefikia sehemu nzuri, wanachama wanajitolea kwa hali na mali, ndani ya siku tatu watajua kiasi kilichopatikana na bado tunawaomba waendelee kujitolea ili klabu yao iendelee kuwa mfano nchini kuanzia uwanjani mpaka umiliki wa vitu vyetu,” alisema Mkwasa.
Aliongeza amekutana na viongozi wanaosimamia eneo la Mto Msimbazi, waliosaidia kutanua mtaro ili kupunguza mafuriko na walimuunganisha wa watu wa Tanroads waliowapa kifusi cha kusaidia ukarabati wa uwanja huo.
“Tanroads wametupa kifusi, tunatafuta namna ya kukifikisha hapa, tayari vifusi vingine vimeishafika na tumesaidiwa namna ya kutanua mtaro wa kupunguza mafuriko kandokando ya uwanja wetu,” alisema Mkwasa.
Post A Comment: