
MBUNGE wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe, ametoa utetezi wake kwa hoja 10 mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, akijibu tuhuma zinazomkabili za kulidhalilisha Bunge katika mitandao ya kijamii.
Zitto alikamatwa na Jeshi la Polisi juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA), akitokea mkoani Kigoma na kupelekwa Dodoma mbele ya kamati hiyo kujibu tuhuma hizo.
Katika taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari baada ya kuhojiwa na kamati hiyo, Zitto alieleza alivyojibu tuhuma zinazomkabili kwa kukiri na kutoa utetezi wake kwa hoja zipatazo 10.
“Leo nimefika mbele yenu na nitajibu wito wenu kama ifuatavyo, kwamba maoni yangu kwenye mtandao wa Twitter kuwa "Bunge siku hizi ni idara ya Tawi la Utawala" yanadhalilisha mhimili wa Bunge”.
“Maneno hayo ni yangu na nimeyatoa kama raia wa Tanzania. Ninaamini kwa dhati kuwa Bunge la 11 limekuwa likifanya kazi kwa kuingiliwa na serikali chini ya Rais John Pombe Magufuli,” alisema Zitto.
Hoja 10 za utetezi
Hoja ya kwanza aliyoitoa Zitto alieleza kuwa hatua ya kuzuiwa kwa matangazo ya bunge kwa kisingizio cha kupunguza gharama za uendeshaji wa mhimili wa Bunge, ni dalili ya wazi ya kufifisha sauti ya Bunge na kupandisha sauti ya serikali.
Hoja ya pili Zitto aliitaja kuwa ni kitendo cha uongozi wa Bunge kurudisha serikalini Sh. bilioni sita bila ridhaa ya wabunge kwa kisingizio kwamba zimebaki kutokana na kubana matumizi.
Hoja ya tatu ya utetezi huo ni maelekezo ya mhimili wa dola kwa Bunge, kupitia maagizo ya Rais John Magufuli kwa Spika Job
Ndugai kuwa "Awashughulikie wabunge aliowaita "waropokaji", ili waje wazungumze nje ya Bunge na yeye Rais (Serikali) apate nafasi ya kuwashughulikia.
Hoja nyingine ni kitendo cha Bunge kuhariri hotuba za kambi ya upinzani kwa kushinikiza kuondolewa kwa vipengele vinavyoikosoa serikali.
“Mathalani, wakati wa Bunge la Bajeti, hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, iliamriwa kuondolewa maneno yanayohusu kashfa ya Mkataba wa Lugumi, kumhusisha Rais na kuuzwa kwa nyumba za serikali, mauaji ya wanasiasa, pamoja na Bunge kulinda wahalifu,” alisema Zitto.
Hoja ya tano ni aliyoitoa ni kauli ya Rais Magufuli aliyoitoa Novemba 4, mwaka jana akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuwa "mzizi wa mhimili wa serikali ni mrefu zaidi kuliko mihimili mingine" baada ya kuulizwa juu ya matumizi ya serikali nje ya bajeti iliyoidhinishwa na bunge.
Hoja nyingine ni kitendo cha Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Tanzanite na Almasi kusomwa nje ya Bunge na kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu na Rais bila kuwasilishwa na kujadiliwa Bungeni , ili kuwekewa azimio la Bunge.
Zitto alisema kitendo hicho kinaifanya kamati hiyo kuonekana kuwa ya serikali badala ya Kamati ya Bunge.
Hoja ya saba ni kauli ya Rais Magufuli kuwa Spika kumpigia simu kumuuliza juu ya wajumbe wa kuwaweka kwenye Kamati za Bunge za Tanzanite na Almasi.
Hoja nyingine ni kitendo cha Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi wakati Bunge likiendelea, wabunge kukamatwa ovyo ni dharau ya hali ya juu kwa mhimili huo.
Zitto alitaja hoja nyingine kuwa ni kitendo cha serikali kutowasilisha taarifa za utendaji wa robo mwaka kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2014.
Hoja ya mwisho aliyoitoa Zitto ni Bajeti ya Bunge kutowekwa kwenye Mfuko wa Bunge kwa mujibu wa sheria na Spika kutakiwa kuomba vibali vya safari za wabunge kwa mkuu wa tawi la utendaji (serikali).
Post A Comment: