
Azam FC jana imefanikiwa kuingia
kwenye fainali ya mashindano ya Kagame Cup baada ya kuiondosha timu KCCA
ya Uganda kwa goli 1-0 kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa jana
jioni katika uwanja wa Taifa.
Azam wameweka rekodi ya kuwa timu
iliyotinga hatua ya fainali ya michuano ya Kagame mwaka 2015 ikiwa
haijaruhusu goli ndani ya dakika 90 huku ikiwa imefunga jumla ya magoli
10 kuanzia hatua ya makundi hadi mchezo wa nusu fainali.
Kutofungwa goli hata moja
inadhihirisha kuwa safu ya ulinzi ya Azam ni bora zaidi ambayo imekuwa
haipenyeki kirahisi na washambuliaji wa timu pinzani pindi wanapokutana.
Ukuta wa Azam ukiongozwa na Pascal Wawa umekuwa imara na hiyo
imepelekea beki huyo (Wawa) kutangazwa kama mchezaji bora wa mechi (man
of the match) mara mbili wakati Manula yeye akiwa amechukua mara moja.
Kesho Azam inakutana na Gor Mahia
ya Kenya kwenye mchezo wa fainali ambao unatabiriwa kuwa ni mchezo
mgumu na wa upinzani mkubwa. Ugumu wa mchezo huo unasababishwa na aina
ya wachezaji wanaokutana kwenye mchezo wenyewe.
Kwa upande wa Gor Mahia, wao
silaha yao kubwa imekuwa ni mshambuliaji wao Michael Olunga ambaye ndiye
anaeongoza kwa magoli hadi sasa akiwa ameshatupia wavuni jumla ya
magoli matano. Olunga ni aina ya mshambuliaji amabae anajua vizuri
kutumia nafasi zinazotengenezwa, anapopata nafasi basi anakuwa ni mtu
hatari sana kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzifumania nyavu.
Kagere Medie, Godfrey Walusimbi
na Haruna Shakava ni wachezaji wengine ambao ni moto wa kuotea mbali kwa
upande wa Gor Mahia na wanahitaji uangalizi wa haili ya juu pindi
wawapo uwanjani kwani wanauwezo mkubwa wa kufanya lolote litakalo badili
matokeo wakati wowote wa mchezo.
Azam wao pia wanawachezaji ambao
ni nguzo ya timu yao na mara nyingi wanaonekana kuibeba timu iwapo
uwanjani. Uwepo wa Pascal Wawa kwenye safu ya ulinzi unaifanya Azam
kutokuwa na presha kubwa kwani Wawa ni mchezaji anaeyatambua vyema
majukumu yake. Kipre Tchetche licha ya kuwa anapoteza nafasi nyingi za
kufunga lakini bado ni mchezaji wa kuogopwa hasa kwenye mchezo wa
fainali.
Farid Mussa ni mlinzi wa kushoto
wa Azam na amekuwa kwenye kiwango bora sana tangu kuanza kwa michuano
hii, anaweza kukaba vizuri na kupandisha mashambulizi pale timu yake
inapokuwa inashambulia. Jana alifunga goli pekee lililoivusha Azam na
kuipeleka kwenye hatua ya fainali ya Kagame, ni mchezaji mwingine wa
kuangaliwa sana na timu ya Gor Mahia.
Mugiraneza licha ya kujiunga na
Azam siku za hivi karibuni ameonekana ni mchezaji ambaye anakipaji cha
hali ya juu hasa anapocheza katika eneo la kiungo wa ulinzi, aweza
kukaba vizuri, anacheza mipira ya juu lakini pia anauwezo wa kupiga pasi
ndefu.
Azam imeingia hatua ya fainali
kwa mbinde kutokana na kupata upinzani wa hali ya juu kutoka kwa KCCA
tofauti na wengi walivyokuwa wanatarajia. Gor Mahia wao wametinga hatua
hiyo kwa ushindi wa goli 3-1 walioupata kutoka kwa timu ngumu na ngeni
kwenye mashindano haya Khartoum ya Sudani.
Kesho kutakuwa na mechi ya
kumpata mshindi wa tatu itakayo zikutanisha timu zilizofungwa jana
kwenye nusu fainali ambazo ni KCCA dhidi ya Khartoum mchezo
utakaotangulia mchana kabla ya fainali ya mashindano hayo kupigwa kati
ya Azam FC dhidi ya Gor Mahia.
Post A Comment: