
MUONEKANO wako mahali popote pale una nafasi kubwa kukupa utambulisho. Utambulisho huo unaweza kuwa mzuri au vinginevyo.
Unakumbuka siku uliyopanga kukutana kwa mara ya kwanza kwa ajili ya maongezi na mtu umpendaye? Unakumbuka siku uliyoitwa kwa ajili ya usaili wa kazi? Bila shaka moja ya vitu vinavyokujia kwenye mawazo yako ni jinsi utakavyoonekana katika siku hiyo adhimu.
Hii haina maana kuwa tunapoenda kazini lazima tupanie kwa ‘viwalo vikali’ kupitiliza kama tunaenda kwenye miadi ya kukutana na mchumba mtarajiwa.
Bali, najirabu tu kukuonyesha kwa lugha ya picha kuwa muonekano wako unaongeza ujasiri na thamani inayoweza kufungua milango mingine mingi.
Watu hupenda kukuweka kwenye kundi fulani kutokana na jinsi unavyoonekana. Hii inamaanisha kwamba tunaweza kuamua ni kundi gani watu watuweke.
Ifahamike kwamba unadhifu siyo kuwa na nguo mpya au za gharama kubwa, ni kuonekana msafi na kuvutia mbele ya wengine.
Kanuni za Maadili na Mwenendo wa Kazi katika sekta ya Umma zinamtaka mfanyakazi kuwa msafi na nadhifu wakati wote.
Miongozo hii au ya aina hii ipo katika ofisi nyingi, hata zile za binafsi, lakini pia ni moja ya mambo ambayo tamaduni za kila jamii kuanzia ngazi ya familia, hutiliwa mkazo.
Je, zipi ni faida za kuwa msafi na nadhifu katika mahala pa kazi? Wacha leo tuzijadili faida sita muhimu:
KUJIONGEZEA USHAWISHI
Nafasi ya kupendwa na kusikilizwa inaongeza zaidi kwa watu wenye
muonekano nadhifu kuliko wale ambao si nadhifu.
Ukitaka kuwa kiongozi vaa kama kiongozi; muonekano wako unakuongezea nafasi kubwa ya kuwavutia wengine. Sisemi uvae suti au mavazi ya gharama kila siku, hapana, lakini muonekano wa mwili na mavazi uwe nadhifu.
KUEPUKA MADHARA YA KINIDHAMU
Kanuni za mashirika mengi zinamuhitaji mfanyakazi kuwa msafi na mwenye muonekano mzuri kila wakati. Wapo wanaokumbana na adhabu za kinidhamu kwa sababu tu ya kukosa muonekano nadhifu kazini.
Zipo ofisi zinazotaka mtu akivaa shati ni lazima achomekee na suala dogo kama hili linapelekea mtu kupata barua ya onyo kwa sababu tu ameshandwa kufuata taratibu ndogo kama hizi. Ni vyema kujiepusha na matatizo ya kinidhamu kwa kushindwa kuheshimu taratibu na miongozo midogo midogo kama hii.
KUJIONGEZEA MARAFIKI KAZINI
Kiuhalisia hakuna mtu ambaye atapenda kuwa na rafiki mwenye harufu kali kutoka sehemu yoyote ya mwili wake na kama yupo sio kitu ambacho atakifurahia kwenye urafiki wao.
Hivyo ili marafiki zako wawe na uhuru wakukaa karibu na wewe au hata wakukumbatia unapoingia kazini jitahidi uwe msafi na nadhifu. Kama hauwezi kufanya kwa ajili yako basi fanya kwa ajili ya wengine.
KUONGEZA HESHIMA
Pamoja na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia hatuwezi kupinga ukweli kwamba maisha yetu hata makazini yanaathiriwa na mila na desturi zetu. Kama nilivyosema awali muonekano wako unaweza kusababisha watu wakuweke kwenye makundi mbalimbali.
Hivyo muonekano wako unaweza kukuongezea au kukupunguzia heshima pia. Nguo fupi kupitiliza, zakubana au zinazonesha maungo ya ndani ya mvaaji vinaweza kutafsiriwa kama utovu wa Nidhamu na kukosa heshima japo sio wote wanaoweza kukwambia ukweli huu.
Japo tamaduni za jamii fulani zinaweza kuathiri maisha yetu maofisini lakini pia kuna tamaduni za taasisi hivyo ni bora kuzingatia yote haya.
MVUTO KWA UNAOWAHUDUMIA
Kanuni za huduma kwa mteja zina mtaka mtoa huduma kuwa na muonekano utakao mpendeza mteja wake. Hii ni kwa wateja wa nje (wanunuzi wa bidhaa/huduma) na wateja wa ndani (wafanyakazi wenzako).
Hii haiishii kwenye unavyovaa au unavyonukia lakini pia unavyoongea na wateja wako.
Wateja wanaweza penda kuhudumiwa na wewe kwa sababu ya uvaaji na tabasamu unalotoa unapowahudumia. Kwa bahati mbaya mvuto huu umekuwa ukitafsiriwa vibaya na wengine kiasi cha kuamua kuvaa nguo zinazoenda kinyumAe na maadili ya tamaduni zetu au hata yale ya kazi pia.
KUONGEZA UJASIRI
Kuwa huru na amani na kile ulichokivaa inasaidia kuongeza ujasiri wako kazini lakini pia kwa wengine kuwa huru na unavyoonekana kuna kupa ujasiri. Unapoamua kuvaa vazi ambalo pengine limekubana sana, fupi sana, halijanyooshwa au lina rangi zinazokela husababisha kupunguza
ujasiri na kujiamini.
Ni vyema kuhakikisha kuwa unakuwa nadhifu muda wote maeneo ya kazi. Usikubali kuharibu siku yako maeneo ya kazi kwa kuvaa kitu kisichokupa amani kwani hii huathiri hata ufanisi wako kazini.
CHANGAMOTO ZA MUONEKANO KAZINI
Linapokuja suala la muonekano kuna changamoto kadhaa ambazo wengi hukabiliana nazo. Watu wengi hutoa sababu ya gharama zinazohusiana na kuwa na muonekano mzuri.
Ukweli ni kwamba fedha ina sehemu ndogo katika kumuweka nadhifu. Kama nilivosema awali hauhitaji kuwa na nguo mpya kuwa nadhifu lakini suala la kufua nguo zako, kuzinyosha,
kusafisha viatu vyako na kuhakikisha nywele zako zinamuonekano mzuri na hautoi harufu za kukera wenzako ni masuala ya kitabia zaidi si sio ya kifedha.
Changamoto nyingine ni suala la mitindo. Mitindo mbali mbali inayokuja hutumiwa na wafanyakazi kwa nia njema lakini wakati mwingine husababisha wafanyakazi kwenda kinyume na maadili ya kazi.
Kuna baadhi ya mitindo ya nywele, mavazi na namna ya kijilemba au kujipodoa hairuhusiwi kwenye baadhi ya ofisi hasa katika ofisi za Umma.
Hivyo ni vyema kuhakikisha pia wafanyakazi wanafuata kanuni na miongozo maeneo ya kazi ili kuepuka usumbufu usio wa lazima Aina ya kazi mtu anayofanya inaweza pia ika athiri muonekano wake.
Wapo wanaota sababu ya aina ya kazi wanazozifanya kama kikwazo cha kutokuwa nadhaifu. Watu wengi wanaofanya shughuli zao kwenye mitambo au maeneo ambayo wanahisi hayahitaji utanashati na unadhifu huifanya hii kama sababu.
Ni ukweli ulio wazi kwamba mazingira ya kazi ya watu wa aina hii yana athari kwenye muonekano wao lakini haizuii wao kuwa nadhifu pia kwani sio muda wote katika eneo la kazi wanakuwa katika mavazi ya shughuli wanazozifanya.
Pamoja na muonekano mzuri kuwa na umuhimu maeneo ya kazi, umuhimu wake upo katika maeneo mengi. Kwa kuzingatia kuwa mara nyingi hili ni suala la kitabia linahitaji mtu binafsi kuelewa umuhimu wake na kujenga mazoea ya kujiweka nadhifu kila wakati. Usikubali haurufu ya domo, kikwapa, viatu na muonekano usiovutia kukunyima uhuru na kufurahia kazi yako – chukua hatua.
Post A Comment: